Na Brian Okoth
Watu kadhaa wamefariki katika kaunti ya kaskazini-mashariki mwa Kenya, Marsabit, baada ya ugonjwa "ajabu" kuzuka katika eneo hilo.
Likinukuu mamlaka za mitaa, gazeti la Nation la Kenya liliripoti kuwa watu tisa walithibitishwa kufariki na wengine 80 wakiugua katika Kijiji cha Kargi, Kaunti Ndogo ya Laisamis.
Grace Galmo, waziri wa afya wa kaunti, hata hivyo aliambia TRT Afrika kwamba idadi rasmi ya waliofariki ni ndogo.
"Vifo viwili vimesajiliwa katika vituo vya afya, lakini idara imepokea ripoti ambazo hazijathibitishwa za vifo vingine vilivyotokea ndani ya jamii," alisema.
Ugonjwa huo ulikuwa na dalili zinazofanana na malaria, vyombo vya habari vya ndani viliripoti
Idara ya afya ilisema imeanza kuchunguza mlipuko huo, na imetuma maafisa wa afya huko Laisamis.
Galmo alisema dawa zaidi zimetumwa Laisamis kusaidia kudhibiti hali hiyo.
"Tunawahimiza wakazi kuchukua hatua za kuzuia kama vile kunawa mikono mara kwa mara kwa sabuni na maji, kuepuka kuwasiliana na wagonjwa na kutafuta matibabu ikiwa watapata dalili zozote," alisema.