Waziri wa Afya wa Rwanda, Dkt Sabin Nsanzimana./Picha: Wengine

Watu sita wamethibitishwa kufa nchini Rwanda kutokana na kuugua maradhi ya Marburg, Waziri wa Afya wa nchi hiyo, Dkt Sabin Nsanzimana amesema.

“Homa kali inayosababishwa na Marburg imegundulika nchini Rwanda. Jumla ya watu 20 wameugua na wengine sita wamepoteza maisha,” alisema Nsanzimana kupitia video iliyowekwa kwenye ukurasa wa Shirika la Habari la Rwanda (RBA).

Kulingana na Nsanzimana, wengi waliopoteza maisha na waliougua ni wafanyakazi wa vituo hivyo vya afya.

Dkt Nsanzimana alisema kuwa ugonjwa huo huambukizwa kwa njia ya damu na maji maji kutoka kwa watu wenye ugonjwa huo.

Pia ameongeza kuwa inaweza kuchukua hadi wiki tatu kwa aliyeambukizwa kutoonesha dalili zozote za ugonjwa huo.

“Ni ugonjwa hatari sana, kiasi kwamba yule aliyeambukizwa anaweza kupoteza uhai,” alisema.

Virusi vya Marburg vinatajwa na wataalamu wa afya kuwa sawa na virusi hatari vya Ebola, vikiwa vimegunduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1967 nchini Ujerumani baada ya watu 9 kuambukizwa na saba kufariki dunia.

TRT Afrika