Mwinjoyo FM iko katika Kaunti ya Nakuru, takriban kilomita 160 kaskazini-magharibi mwa mji mkuu wa Kenya, Nairobi. Picha: Getty

Polisi Nakuru, kaunti ya eneo la Rift Valley, nchini Kenya, wameanzisha msako wa kuwakamata watu kutoka kundi moja linalodaiwa kuwaibia watangazaji wa vituo vya redio Alhamisi usiku.

Watangazaji wawili wa Mwinjoyo FM katika Kaunti ya Nakuru walikuwa hewani mubashara, wakati watu watatu waliokuwa wamejihami wakiwa wamevaa barakoa walipovamia studio na kuwaambia walale chini.

Watuhumiwa hao waliokuwa na bunduki aina ya AK-47, pia waliamuru kwamba masafa ya kituo hicho zizimwe.

Tukio hilo lilinaswa kwenye matangazo ya Facebook Live ya Mwinjoyo FM kwa dakika tatu.

Walipogundua kuwa vitendo vyao viliangaziwa kwa mamia ya wafuasi, washukiwa walichukua simu za mkononi za watangazaji na kuzima matangazo ya moja kwa moja.

Afisa wa Kurugenzi ya Upelelezi wa Jinai wa Nakuru Mashariki, DCIO, George Momanyi aliiambia TRT Afrika kwamba uchunguzi kuhusu tukio hilo umeanza.

Nakuru, mji mkuu ambao ulipata hadhi ya jiji hivi majuzi, uko kilomita 160 Kaskazini Magharibi mwa mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

TRT Afrika na mashirika ya habari