Takriban wanajeshi 23 wa Congo wanakabiliwa na hukumu ya kifo au kifungo cha miaka 10 hadi 20 gerezani kufuatia kufikishwa mahakamani Jumatatu kwa tuhuma za ubakaji, kutoroka vita na uhalifu mwingine wakati wa mapigano mashariki mwa nchi hiyo yenye mizozo, kulingana na jeshi la Kongo.
Wanajeshi hao walifikishwa mbele ya mahakama ya kijeshi katika eneo la Butembo katika jimbo la Kivu Kaskazini, kwa mujibu wa msemaji wa jeshi Lt. Kanali MaK Hazukay. Vikosi vya usalama vimekuwa vikipambana na zaidi ya vikundi 120 vya waasi katika eneo hilo lenye utajiri wa madini kwa miaka mingi.
DRC iliondoa usitishaji wa zaidi ya miaka 20 wa hukumu ya kifo mwezi Machi, uamuzi uliokosolewa na wanaharakati wa haki.
Mnamo mwezi Mei, wanajeshi wanane walihukumiwa kifo kwa kukimbia uwanja wa vita, na mnamo Julai, wanajeshi 25 walipatikana na hatia ya makosa kama hayo. Hakuna hata mmoja wao aliyethibitishwa kunyongwa.
Askari kumi kati ya waliofikishwa mahakamani Jumatatu wanafunguliwa mashitaka ya kutoroka, ambayo ina adhabu ya kifo, huku wengine wakikabiliwa na mashtaka ya kutumia vibaya silaha za kijeshi, kutotii, wizi na ubakaji, msemaji wa jeshi aliambia Associated Press.
Waasi wa M23
Mashariki mwa Congo, inayopakana na Rwanda na Uganda, kwa muda mrefu imekuwa ikikabiliwa na ghasia za kutumia silaha huku waasi wakipigania mamlaka, ardhi na rasilimali za madini, huku wengine wakijaribu kutetea jamii zao.
Miongoni mwa makundi ya waasi wanaofanya kazi katika eneo hilo ni M23, ambayo Umoja wa Mataifa na serikali ya Congo wanasema inaungwa mkono kwa silaha na wanajeshi na Rwanda.
Rwanda imekanusha kuhusika katika mzozo huo ambao umezua mojawapo ya majanga makubwa zaidi ya kibinadamu duniani, huku zaidi ya watu milioni 7 wakiwa wamekimbia makazi yao.