Mradi wa ujenzi ukiendelea nchini Nigeria./Picha: Getty

Na Edward Qorro

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Wanaigeria waishio na kufanya kazi ughaibuni wanaongoza kwa kutuma pesa nchini mwao, kulingana na utafiti uliofanywa na KNOMAD.

Taasisi ya KNOMAD inaelezea fedha kama kiasi kinachotumwa nyumbani kama sehemu ya kipato au ujira kutoka kwa raia wanaofanya kazi nje ya nchi zao.

Nchi hiyo inayopatikana Magharibi mwa Bara la Afrika, inasifika kwa kuwa na idadi kubwa ya watu, wanaokadiriwa kufikia zaidi ya milioni 200, wakiwa wametawanyika sehemu mbalimbali duniani.

Ghana inashika nafasi ya pili, raia wake wakiwa wametuma nyumbani jumla ya Dola bilioni 4.9, kulingana na utafiti wa KNOMAD.

Jumla ya Dola bilioni 4.2 zilitumwa na Wakenya waishio ughaibuni, utafiti huo umeongeza.

"Sehemu ya kusini mwa jangwa la Sahara imeshuhudia mwendeno huu huku fedha zinazotumwa katika eneo hilo zikiongezeka kwa zaidi ya asilimia 55," imesomeka sehemu ya utafiti huo.

Wakati Zimbabwe ikipokea Dola bilioni 3.1 kutoka kwa raia wake, Wasenegali walituma Dola bilioni 2.9 nchini mwao kutokana na shughuli zao ughaibuni.

Umoja wa Mataifa unasema kwamba mtu mmoja kati ya tisa duniani kote ni mnufaika wa fedha zinazopokelewa kutoka nje ya nchi, na nusu ya kiasi hicho kinaishia katika maeneo ya mashambani, ambako baadhi ya watu maskini zaidi duniani wanaishi. Hii pia inafanya fedha zinazotumwa kutoka nje kuwa muhimu mara tatu zaidi ya misaada ya kimataifa.

DRC ilitia kibindoni Dola bilioni 1.4 kutoka kwa raia wake waishio nje ya nchi hiyo inayopatikana katika ukanda wa Afrika Mashariki wakati majirani zao wa Uganda walichangia Dola bilioni 1.3.

Kwa mujibu wa utafiti huo, raia wa Mali walituma Dola bilioni 1.2 nyumbani wakati nchi ya Sudan ilipokea Dola bilioni 1.0, huku wananchi wa Afrika Kusini walipeleka nchini mwao Dola bilioni 0.8.

TRT Afrika