Wakenya mtandaoni (KOT) wameitisha maandamano ya nchi nzima Jumanne Oktoba mosi, wakidai kuachiliwa kwa mwanaharakati Morara Kebaso.
Morara, ambaye ni wakili aliyegeuka kuwa mwanaharakati, anadaiwa kukamatwa akiwa ofisini mwake kitongoji cha Kahawa jijini Nairobi.
Walioshuhudia kukamatwa kwake wanadai kuwa watu waliovaa mavazi ya kiraia wakiwa na bunduki walivamia ofisi za Morara Jumatatu mwendo wa saa nane mchana na kumkamata na kumtia kwenye gari na kuondoka naye bila kusema amekamatwa kwa makosa gani.
Washirika wa Morara walionyesha video mtandaoni wakiwa wanafuata kwa kasi magari ya maafisa wa upelelezi, katika kile kilionekana kama mchezo wa paka na panya, wakidai wanahofia Morara anahamishiwa eneo lisilojulikana.
''Fuata gari hilo na usikubali likupotee, mimi nitamfuata huyu wa geri nyeupe'' anasikika mmoja wa washirika katika gari akimuagiza dereva wa gari la pili, pale magari waliokuwa wakifuata yalipotawanya njia.
Baadaye taarifa za polisi zilidai kuwa Morara amepelekwa kituo cha Pangani kati kati mwa jiji la Nairobi, lakini wafuasi wake wamekita kambi usiku kucha nje ya makao makuu ya polisi eneo la Upper hill wakisisitiza amefichwa huko.
Ukosoaji wa serikali
Morara Kebaso amegonga vichwa vya habari katika miezi ya hivi karibuni, kutokana na ufuatiliaji wa miradi ya serikali ambayo anadai yamekwama au ni miradi hewa.
Hii imempatia ufuasi mkubwa mitandaoni kutoka kwa Wakenya ambapo wamechukua kurasa zake kama chanzo cha habari za miradi za serikali zinazogharimu mamilioni ya dola.
Katika video yake ya mwisho aliyochapisha katika mtandao wa Tiktok, Morara alionekana kukemea utekaji na ubakaji wa mwanablogi mmoja wa jijini Mombasa, Pwani ya Kenya kutokana na matamshi yake makali dhidi ya uongozi wa kaunti hiyo.
Uchunguzi wa uhalifu huo unaendelea na watu kadhaa tayari wamekamatwa kuhusiana na hilo.
Hata hivyo Morara amedai katika video yake kuwa hatua za polisi hazitoshi huku akitoa makataa kwa Inspekta wa polisi kupanua uchunguzi wake hadi kwa viongozi walioshutumiwa kuhusika.
Polisi hadi sasa hawajatoa taarifa juu ya kukamatwa kwa Morara.
Visa vya utekaji nyara vimezua tetesi kubwa nchini Kenya tangu kuzuka kwa maandamano ya Gen Z mwezi Juni.
Watu kadhaa walitekwa na watu waliodai kuwa maafisa wa polisi, japo haikujulikana walipelekwa wapi na wengine walidaiwa kuzuiwa bila kufunguliwa mashtaka.