Wabunge hao watatu walidaiwa kumtaka mkuu wa Tume ya Haki za Kibinadamu ya Uganda kuongeza bajeti ya shirika hilo ili wanufaike kinyume cha sheria. / Picha: Picha za Getty

Wabunge watatu wa Uganda wameshtakiwa kwa makosa yanayohusiana na rushwa, kwa mujibu wa karatasi ya mashtaka iliyoonwa na Reuters siku ya Jumamosi, huku serikali ya Rais Yoweri Museveni ikiongeza msako dhidi ya ufisadi uliokithiri miongoni mwa wabunge.

Wabunge Michael Mawanda Maranga, Ignatius Wamakuyu Mudimi na Paul Akamba walifikishwa kortini Ijumaa jioni na kushtakiwa kwa "kutorosha rasilimali za umma," karatasi ya mashtaka ilisema.

Wote ni wanachama wa chama tawala cha National Resistance Movement (NRM).

Wote watatu walikana mashtaka na wakarudishwa gerezani.

'Njama ya kulaghai serikali'

Waendesha mashtaka waliwashutumu wabunge watatu kwa kuelekeza takriban shilingi bilioni 3.4 za Uganda (dola 908,605), kwenda "madhumuni yasiyohusiana na yale ambayo rasilimali zilikusudiwa."

Zaidi ya hayo, washukiwa hao watatu pia wanadaiwa "kula njama ya kudanganya serikali ya Uganda", karatasi ya mashtaka ilisema.

Mmoja wa mawakili wao Caleb Alaka alilalamika mahakamani kwamba haki za kikatiba za washukiwa hao zimekiukwa.

Akamba alikuwa tayari ameshtakiwa kwa makosa yanayohusiana na ufisadi wiki jana na kuwekwa rumande, pamoja na wabunge wengine wawili.

Walishutumiwa kwa kujaribu kumshawishi mwenyekiti wa Tume ya Haki za Kibinadamu ya Uganda (UHRC) inayofadhiliwa na serikali kuongeza bajeti ya shirika ya 2024/25 (Julai-Juni), ili kuwapa wabunge 20% ya bajeti iliyopanda.

TRT Afrika