Wabunge wa upinzani nchini Uganda, wametaka Mkuu wa Jeshi la nchini hiyo (UPDF) Jenerali Muhoozi Kainerugaba kuchukuliwa hatua za kinidhamu kufuatia kauli yake aliyoitoa hivi karibuni.
Wanasiasa hao wamestaajabishwa na uamuzi wa Jenerali Muhoozi, kujihusisha na siasa za vyama, baada ya kutamka wazi kuwa hakuna raia nchini Uganda atakayeruhusiwa kushika hatamu ya madaraka kutoka kwa Rais Yoweri Museveni, ambaye ameiongoza nchi hiyo toka mwaka 1986.
Katika chapisho aliloliweka kwenye ukurasa wa X, Jenerali Kainerugaba, alitengua nia yake ya kugombea urais mwaka 2026, badala yake ametangaza kumuunga mkono baba yake ambaye ni Rais wa nchi hiyo, Yoweri Museveni katika kinyanganyiro hicho.
Machi 2023 kiongozi huyo wa jeshi nchini humo kupitia mtandao wake wa kijamii wa X alionesha nia ya kugombea nafasi hiyo kuchuana na baba yake.
Hata hivyo, mbunge wa Kira Ibrahim Ssemujju Nganda alisisitiza kuwa kauli za Muhoozi zinakinzana na misingi ya katiba ya Jamhuri ya Uganda.
“Kiongozi wa jeshi anamuunga mkono mgombea kutoka chama cha siasa. Lakini pia, anatoa vitisho kuwa hakuna raia atakayekuja kuwa Rais baada ya baba yake na kwamba jeshi haliwezi kuruhusu hilo lifanyike,” aliongeza.
Hata hivyo, jaribio la mbunge wa Busiro Mashariki, Medard Sseggonato la kumchunguza Jenerali Muhoozi, lilizimwa na Naibu Spika Thomas Tayebwa, ambaye alisema kuwa masuala ya kijeshi ni lazima yaachwe kwa Wizara ya Ulinzi na UPDF.
“UPDF ina kanuni na miiko yake, yoyote atakaye kiuka miiko hiyo basi atachukuliwa hatua. Sitaki kuruhusu bunge liwe chombo cha uchunguzi,” alisema Tayebwa.