Waandishi wa habari jijini Nairobi Jumatano wamepanga kufanya maandamano ya amani kupinga ukatili wa polisi unaowalenga wanahabari wanaoripoti maandamano dhidi ya serikali na aina nyingine za vitisho.
Maandamano hayo yameandaliwa chini ya mwamvuli wa Chama cha Wahariri wa Kenya (KEG), pamoja na Muungano wa Wanahabari wa Kenya (KUJ) na wadau wengine 20 wa vyombo vya habari nchini Kenya.
''Wanahabari wote na watetezi wa haki za binadamu wanalaani mashambulizi na unyanyasaji unaowalenga wanahabari na vitisho vyote kwa uhuru wa vyombo vya habari kama inavyothibitishwa na Katiba yetu,'' ilisema taarifa ya wahariri hao.
Kukamatwa kwa mwanahabari mkongwe Macharia Gaitho mnamo Julai 17, 2024, ambako polisi walikiri baadaye kuwa ni kisa cha utambulisho usio sahihi, na kupigwa risasi kwa Catherine Wanjeri Kariuki, mwanahabari wa televisheni na redio mjini Nakuru, siku moja kabla, kuliibua wito wa kuandamano.
''Leo, wafanyakazi wa vyombo vya habari wanatumia haki zao kama raia na wanataaluma kujumuika pamoja na kuonyesha hasira zetu kuhusu unyanyasaji wa polisi dhidi ya waandishi wa habari, vitisho vya kufunga makampuni ya vyombo vya habari, na mbinu nyengine za kizamani zinazotumiwa na mashirika ya serikali na wanasiasa wanaotaka kuzuia uhuru wetu tulioupata kwa bidii,'' Naibu rais wa Chama cha Wahariri nchini Kenya (KEG) Ruth Nesoba ameambia TRT Afrika.
Waandishi hao wataandamana hadi Jogoo House kuwasilisha ombi kwa Kaimu Inspekta Jenerali Douglas Kanja na kisha kuelekea Teleposta Towers kuwasilisha ombi hilo hilo kwa Wizara ya Habari na Mawasiliano.
''Lengo kuu leo ni kutetea uhuru wa vyombo vya habari na usalama wa wanahabari,'' anasema Mhariri Nesoba. ''Polisi wanapotumia nguvu kupita kiasi dhidi ya wanataaluma wa vyombo vya habari ambao wanafanya kazi zao tu, hutuma ujumbe wa kutisha na kutishia uwezo wa waandishi wa habari kuwawajibisha walio madarakani,'' Nesoba anaambia TRT Afrika.
Waandishi hao wameorodhesha matakwa muhimu wanayotaka yaangaziwe kwa haraka na wakuu wa vyombo vya usalama na mamlaka ya mawasiliano.
Miongoni mwa matakwa yao :
- Uwajibikaji wa ufyatuaji risasi haramu, kupigwa, kutekwa nyara na kunyanyaswa kwa waandishi katika wiki chache zilizopita, maelezo ambayo yako hadharani.
- Maafisa wa polisi walaghai wafunguliwe mashtaka kwa uhalifu dhidi ya wanahabari na waandamanaji wasio na hatia.
- Uhakikisho wa usalama wa wanahabari wote wanaofanya kazi nchini kutokana na vitisho vilivyotolewa na maafisa wa serikali.
- Kukomesha vitisho vilivyofichwa vilivyotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano na vyombo vyengine vya dola, ambavyo vimezua hofu na hivyo kutishia uhuru wa vyombo vya habari.
- Hakikisho kwamba Wizara ya Habari, Mawasiliano, na Uchumi wa Dijitali itakoma kuingilia uhuru wa taasisi za habari.
- Malipo ya mara moja ya madini yaliyosalia yanayodaiwa na vyombo vya habari, ikiwa ni pamoja na kusitisha matumizi ya matangazo ya serikali ili kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari.
- Kukomesha Udhibiti wa vyombo vya habari.
- Marejeleo ya dhamira ya serikali kwa utawala wa sheria nchini na haswa kwa uhuru wa vyombo vya habari.