Maandamano yamefanyika katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu kupinga mauaji ya Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas Ismail Haniyeh na Israel.
Wanafunzi, wafanyabiashara na viongozi wa kidini walijitokeza mjini Mogadishu kuonyesha mshikamano na watu wa Palestina ambao wamekuwa wakikabiliwa na mashambulizi ya Israel huko Gaza na Ukingo wa Magharibi tangu shambulio la Oktoba 7 lililofanywa na kundi la muqawama la Palestina, Hamas dhidi ya Israel.
Waandamanaji waliongozwa na mwanazuoni maarufu wa Kiislamu wa Somalia Sheikh Abdi Hayi ambaye alimsuta Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wakati wa mikutano ya Ijumaa.
"Hakuna Mungu ila Allah, Netanyahu ni adui wa Allah," waandamanaji waliimba.
Hofu ya kuongezeka mgogoro
Serikali ya Somalia ililaani vikali mauaji ya Haniyeh siku ya Jumatano na kusema ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.
Haniyeh, ambaye alikuwa katika mji mkuu wa Iran wa Tehran kwa ajili ya kuapishwa kwa Rais Masoud Pezeshkian, aliuawa kwa shambulio la anga lililolenga jengo alimokuwa akiishi.
Hamas na Iran zimeilaumu Israel kwa shambulio hilo lakini Tel Aviv haijadai wala kukana kuhusika.
"Somalia inahofia kuongezeka kwa kasi ya vurugu ambayo inaweza kusababisha ukiukwaji zaidi dhidi ya raia," ilisema Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia, ikitoa "rambirambi za moyo" kwa watu wa Palestina.
Mogadishu inalaani mauaji ya kisiasa na ghasia "katika aina zake zote, bila kujali nia yake ni nini," ilisema katika taarifa.