Kombe la dunia U-20 limefikia nusu fainali bila timu hata moja ya Afrika. Afrika iliachwa bila nchi ya kushabikia baada ya kuondolewa kwa Nigeria waliokuwa timu ya pekee iliyoingia robo fainali ya kombe hilo nchini Argentina.
Flying Eagles walitawala muda wote wa dakika 90 za mechi, lakini juhudi zao hazikufua dafu walipokosa kutikisa wavu wa wapinzani wao.
Mabingwa hao kutoka Asia walitumia fursa ya dakika za ziada kujinyakulia bao moja na kuhakikisha wamezima matumaini yoyote ya Nigeria kwenda mbele.
Bao la Choi lilimpukusa kipa wa Nigeria Aniagboso na kumpita kutulia wavuni.
Korea Kusini sasa wamejiwekea miadi ya Italia, ambao walifika hapa kwa kuimiminia Colombia mabao matatu na kuonesha namna wao ndio vigogo wa kuogopewa katika mchuano huu.
Mara ya Mwisho timu ya Afrika kunyakua kombe hilo ni 2009 baada Ghana kuicharaza Brazil 4-3 katika mikwaju ya Penalti.
Fainali ya kombe hili itachezwa Juni 12.