Mwenyeji wa mkutano wa kimataifa wa tabia nchi unaoendelea jijini Nairobi William Ruto amesema kuwa nchi yake inaendeleza juhudi za kuwaondolea vikwazo raia wa nchi za kigeni haswa wanaolenga kuzuru Kenya, kwani ndio nyumbani.
Ruto, akiwahutubia wajumbe wa Mkutano mkuu wa hali ya hewa barani Afrika jijini Nairobi, alisema sio haki kutafuta idhini ya visa kwa "yeyote anayerudi nyumbani".
"Tunafanya mazungumzo kama Wakenya kwamba baada ya miezi michache, tunazingatia kwa dhati kukomesha mahitaji yoyote ya VISA kwa sababu si haki kumuuliza viza mtu yeyote anayerejea nyumbani," rais Ruto alisema.
Kenya imefanya makubaliano ya kuodoa mahitaji ya viza kwa Indonesia, Senegal na Congo katika miezi ya hivi karibuni na makubaliano sawa na hayo na Comoro pia yanapangwa kuanza mwishoni mwa mwaka huu.
“Ninaahidi ya kwamba hii ni mara ya mwisho kutafuta visa ya kuja Kenya kwa sababu mbili. Kwanza, kwa sababu hapa ni nyumbani na pili, tunaunga mkono kwa moyo wote AFCFTA. Ni lazima tuondoe vikwazo vyovyote kwa harakati za watu kuzunguka bara letu,” Ruto aliongeza.
Aidha, mapema mwaka huu, Rais William Ruto alizitaka nchi za Afrika kuondoa vizuizi vya usafiri kutoka nchi moja hadi nyingine na kufikiria upya mfumo wao wa visa ili kuimarisha biashara ya ndani ya Afrika na kuweka bara la Afrika tayari kwa mabadiliko ya kweli.
“Watu walioanzisha visa barani Afrika weneyewe wamezitelekeza. Katika bara Ulaya leo, raia wa nchi 27 za Umoja wa Ulaya hawahitaji visa kusafiri kutoka nchi moja hadi nyingine, "alisema.
Mnamo 2017, serikali ya Kenya ilitangaza utoaji wa viza kwa raia wa nchi za kiafrika pindi wanapotua nchini Kenya.
Zaidi ya marais na wakuu wa nchi 20 wa sasa na wa zamani ni miongoni mwa wajumbe 30,000 walioko mjini Nairobi kuhudhuria mkutano juu ya mabadiliko ya tabia nchi.