Shirika la misaada la kimatibabu MSF linasema kuwa limelazimika kusitisha kazi katika kambi kubwa ya watu waliokimbia makazi yao ambapo njaa imethibitishwa katika jimbo la Darfur Kaskazini mwa Sudan, na kuweka maelfu ya watoto wenye utapiamlo katika hatari ya kifo.
MSF ilisema ililazimika kusitisha shughuli katika kambi ya Zamzam kufuatia kuzuiwa kwa msaada karibu na El-Fasher na vikosiu vya Rapid Support Forces (RSF), ambalo limekuwa likizingira jiji hilo kwa miezi kadhaa, pamoja na hujuma za jeshi la Sudan katika utoaji wa msaada maeneo yaliyo nje ya udhibiti wake.
Jeshi na RSF zimekuwa kwenye migogoro kwa karibu miezi 18, na kusababisha mzozo mkubwa wa kibinadamu ambapo zaidi ya watu milioni 10 wamefukuzwa kutoka kwa makazi yao na mashirika ya Umoja wa Mataifa yamejitahidi kutoa misaada.
"Kwa sababu ya vizuizi vya ugavi MSF imelazimika kuacha kuunga mkono kambi ya Zamzam na kuwaacha watoto 5,000 ambao wana utapiamlo, ikiwa ni pamoja na watoto 2,900 ambao wana utapiamlo mkali, bila msaada," Claire San Filippo wa MSF aliambia mkutano Ijumaa.
"Inavunja moyo kulazimika kusimamisha shughuli zetu," alisema.
Njia salama
RSF ilitoa video siku ya Ijumaa ambapo ilisema ilikuwa inahakikisha njia salama kwa raia huko El-Fasher na kutoa vifaa kwa watu waliohamishwa. Hapo awali jeshi limekanusha kuzuia misaada ya kibinadamu.
Mazungumzo yaliyoongozwa na Marekani nchini Uswizi mwezi Agosti yalitoa ahadi kutoka kwa pande zote zinazozozana kuboresha upatikanaji wa misaada. Lakini chini ya malori 200 ya msaada yameingia Darfur kutoka Chad kupitia njia kuu tangu katikati ya Agosti, wakati watu 450,000 wanaoishi Zamzam pekee wanahitaji lori 100 za chakula cha msaada kwa mwezi, kulingana na MSF.
San Filippo pia alisema wafanyakazi wanaofanya kazi na uhaba mkubwa wa vifaa katika hospitali inayofadhiliwa na MSF katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum, wameona ongezeko kubwa la visa vya kiwewe vya vurugu vilivyofika baada ya kuongezeka kwa mapigano hivi karibuni, pamoja na viwango vya juu sana vya utapiamlo.
Wafanyikazi wa matibabu walikuwa wakitukanwa, kunyanyaswa na kushambuliwa walipokuwa wakifanya kazi, aliongeza.
Njaa kwenye kambi
Mfuatiliaji wa njaa anayetambuliwa kimataifa alithibitisha mnamo Agosti kuwa njaa ilikuwa ikitokea Zamzam na kwamba kulikuwa na hatari ya njaa katika maeneo mengine 13 kote Sudan.
"Kwa kweli tuna wasiwasi kwamba maelfu ya watoto wataachwa kufa kama hakuna kitakachofanyika," San Filippo alisema, akitoa wito kwa Umoja wa Mataifa na jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua.
"Kuna haja ya kuongezwa kwa kasi kubwa hivi sasa. Watu wa Sudan hawawezi kusubiri."