Rais Hage Geingob aliiongoza  nchi hiyo ya kusini mwa Afrika tangu 2015/ Picha : Ikulu Tanzania

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameungana na viongozi wengine wa Afrika kutuma salamu za rambirambi kwa jamaa, ndugu na wananchi wa namibia kwa kufiliwa na Rais wao Hage Geingob Jumapili.

''Pumzika kwa amani ndugu yangu mpendwa Hage Geingob,'' Rais Samia aliandika katika mtandao wake wa X, zamani twitter.

Katika taarifa iliyochapishwa katika ukurasa wa X wa Ikulu, Rais Samia alizungumzia urafiki wa muda mrefu na Marehemu rais Geingob ambaye alimuita kaka.

''Nimesikitishwa sana na msibwa wa rafiki yangu Rais wa Namibia Dkt Geingob, ambaye nimemfahamu kuwa kiongozi msikivu, mtu wa watu na amekuwa miongoni mwa alama za ukombozi wa Namibia,'' Rais Samia alisema.

Afrika Kusini

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini alielezea katika mtandao wa X kuwa anaungana na taifa dada kumuomboleza kiongozi, mzalendo na rafiki wa Afrika Kusini.

''Rais Geingob alikuwa mnara mkubwa wa ukombozi wa Namibia kutoka kwa ukoloni na ubaguzi wa rangi,'' alisema Rais Ramaphosa. ''Pia alikuwa na ushawishi mkubwa katika mshikamano ambao watu wa Namibia walieneza kwa watu wa Afrika Kusini ili tuwe huru leo.'' aliongezea kusema.

Namibia inajiandaa kufanya uchaguzi baadaye mwaka huu 2024/ Picha X- Ramaphosa

Kenya

Kwa upande wake Rais wa Kenya William Ruto alisema anatuma rambirambi na pole kwa familia na watu wa Namibia huku akimkumbuka marehemu Rais Hage Geingob kama kiongozi mashuhuri aliyetumikia watu wa Namibia kwa umakini na kujitolea.

''Alikuwa muumini wa Afrika iliyounganishwa na alikuza sana sauti na mwonekano wa bara hili katika nyanja ya kimataifa,'' aliandika Rais Ruto.

Zimbabwe

Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe pia alimkumbuka ndugu yake wa Namibia kama kiongozi thabiti aliyejali wananchi wake.

''Rambirambi zangu za dhati kwa familia ya Rais Hage Geingob na watu wa Namibia. Uongozi na uthabiti wa Rais Geingob utakumbukwa,'' alisema. ''Roho yake ipumzike kwa amani. Maombi yetu yako na Namibia wakati huu mgumu,'' aliendelea kusema.

Serikali ya Namibia haikutoa maelezo zaidi juu ya kilichosababisha kifo cha Rais wake japo anaaminiwa alikuwa anapokea matibabu kwa maradhi ya saratani/ Picha : Rais Mnangagwa.

Somalia

Naye Rais wa Somalia Hassan Sheih Mohamud alimsifia Marehemu Rais Geingob kama kiongozi mashuhuri aliyejitolea maisha yake kuwatumikia watu wake na alikuwa sauti ya kuheshimiwa katika bara la Afrika.

''Katika kipindi hiki kigumu, tunasimama kwa mshikamano na familia yake na watu wa Namibia wanapoomboleza kuondokewa na kiongozi mkuu,'' alisema Rais Mohamud.

Rais wa Namibia Hage Geingob, 82, alifariki hospitalini mapema Jumapili, ofisi ya rais ilisema, wiki kadhaa baada ya kugundulika kuwa na saratani.

Geingob alikuwa akiiongoza nchi hiyo ya kusini mwa Afrika tangu 2015, mwaka ambao alitangaza kuwa amepona saratani ya tezi dume.

Makamu wa Rais Nangolo Mbumba anachukua usukani nchini Namibia hadi uchaguzi wa rais na wabunge mwishoni mwa mwaka huu.

TRT Afrika