Sudan

Mzozo nchini Sudan umeingia wiki ya tatu bila dalili za usitishaji vita wa kudumu au mazungumzo ya kuumaliza. Mapigano zaidi yameripotiwa Jumapili asubuhi katika mji mkuu Khartoum na mji wa Omdurman.

Vita vya kugombea madaraka vimeitumbukiza nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika katika machafuko na wasiwasi wa kimataifa unaongezeka juu ya madhara ya mapigano hayo.

Wito na juhudi za kimataifa ikiwa kutoka Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na kundi la kanda ya Afrika Mashariki, IGAD, kupata vikosi viwili vya jeshi na RSF kusitisha ghasia hadi sasa zimeanza kuzalisha matunda.

Siku ya Jumamosi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, kwa mara nyingine tena alitoa wito wa kukomeshwa kwa umwagaji damu akihimiza uungwaji mkono kwa juhudi zinazoendelea za amani zinazoongozwa na Afrika.

Lakini mapigano makali yalitikisa tena mji mkuu wa Sudan Khartoum siku ya Jumapili huku makumi ya maelfu wakikimbia ghasia hizo za umwagaji damu.

Vikosi vya jeshi vilipambana na wanamgambo katikati mwa jiji la Khartoum licha ya usitishaji wa hivi karibuni wa mapigano, ambao ulitarajiwa kumalizika mwishoni mwa Jumapili.

"Kumekuwa na mapigano makali sana na milio ya risasi kubwa kila baada ya dakika chache tangu asubuhi na mapema mtaani kwangu," shirika la habari la AFP lilimnukuu mkazi wa kusini mwa Khartoum akisema.

Idadi ya vifo inaongezeka

Mapigano yaliripotiwa kuzunguka makao makuu ya jeshi katikati mwa Khartoum, na jeshi pia lilifanya mashambulizi ya anga katika mji pacha wa Omdurman katika mji mkuu wa Mto Nile.

Wakati huo huo, idadi ya vifo kutokana na mapigano yanayoendelea kati ya jeshi na Rapid Support Forces, RSF, imeongezeka hadi 528, kulingana na Wizara ya Afya. Waziri Mkuu wa zamani Abdalla Hamdok alionya vita vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika kuwa na athari kubwa ulimwenguni.

Taarifa ya wizara ilisema kuwa watu 4,599 pia wamejeruhiwa katika ghasia zilizoanza Jumamosi Aprili 15.

Wizara hiyo hapo awali iliweka idadi ya waliofariki kutokana na ghasia zinazoendelea kuwa 512 na wengine 4,193 kujeruhiwa.

Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo Jumamosi jioni, majimbo 12 kati ya 18 ya Sudan yameshuhudia mapigano kati ya pande hizo mbili zinazohasimiana.

Takriban watu 75,000 wamekimbia makazi yao kutokana na mapigano katika mji mkuu Khartoum na pia katika majimbo ya Blue Nile na Kordofan Kaskazini, pamoja na eneo la magharibi la Darfur, kulingana na UN.

Mapigano yameendelea kati ya jeshi la Sudan na wapiganaji wa RSF licha ya kusitishwa kwa mapigano kwa siku tatu.

Katika taarifa, RSF ilidai kuidungua ndege ya kijeshi huko Omdurman, mji pacha wa Khartoum siku ya Jumamosi.

Hakukuwa na maoni yoyote kutoka kwa jeshi la Sudan juu ya madai hayo.

Maelfu ya watu wakiwemo wageni wameikimbia Sudan tangu kuzuka kwa ghasia kati ya pande hizo mbili zinazozozana.

Kulikuwa na kutoelewana kumezuka katika miezi ya hivi karibuni kati ya jeshi na wanamgambo kuhusu mageuzi ya usalama wa kijeshi.

Mageuzi hayo yanatazamia ushiriki kamili wa RSF katika jeshi, mojawapo ya masuala makuu katika mazungumzo ya pande za kimataifa na kikanda kwa ajili ya mpito kwa utawala wa kiraia, wa kidemokrasia nchini Sudan.

TRT Afrika na mashirika ya habari