Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa, alisema "hakuna ratiba" ya kujiondoa katika majimbo ya Kivu Kaskazini au Ituri/ Picha : Reuters 

Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya congo utasitisha uondoaji wake, bila ratiba iliyowekwa kwa awamu inayofuata baada ya ile ya awali mwezi Juni, serikali na ujumbe huo ulisema.

Mwezi Septemba mwaka jana, Rais Felix Tshisekedi aliuomba ujumbe huo kuharakisha uondoaji wa askari wa kulinda amani waliotumwa katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati ili kuzima hali ya ukosefu wa usalama unaosababishwa na makundi yenye silaha yanayopigania ardhi na rasilimali.

Awamu ya kwanza ya uondoaji huo, katika jimbo la Kivu Kusini, ilikamilika Juni 25, balozi wa congo katika Umoja wa Mataifa, Zenon Mukongo Ngay, alisema Jumatatu. Ilikuwa imepangwa kukamilika ifikapo Aprili.

Ngay alidokeza kuwa masharti bado hayajatimizwa kwa awamu inayofuata, hata hivyo, akiilaumu nchi jirani ya Rwanda kwa kuzidisha mapigano mashariki mwa Kongo.

"Kwa kuzingatia kuendelea kwa uchokozi wa Rwanda huko Kivu Kaskazini, awamu inayofuata ya kujiondoa, awamu ya 2, itafanywa wakati hali itakaporuhusu, kufuatia tathmini zinazoendelea za pamoja," alisema katika hotuba yake katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Congo na Umoja wa Mataifa kwa muda mrefu wamekuwa wakiishutumu Rwanda kwa kuunga mkono kundi la waasi la M23, madai ambayo Kigali imekanusha.

Bintou Keita, mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa, alisema "hakuna ratiba" ya kujiondoa katika majimbo ya Kivu Kaskazini au Ituri.

"Usiniulize nini kitafuata," Keita aliwaambia waandishi wa habari katika Umoja wa Mataifa mjini New York siku ya Jumatatu. "Nini kinachofuata, kama tulivyosema, (ni) tunasimama, tunajiandaa, na tunaona kitakachofuata kulingana na hali halisi iliyopo."

Waziri wa mambo ya nje wa Kongo Therese Wamba Wagner alisema serikali inataka kuepusha kuleta pengo la usalama.

"Inapokuja Kivu Kaskazini, tutatilia maanani maendeleo tunayoyaona kabla ya kufanya maamuzi yanayowajibika na kuanza mchakato huu wakati hali nzuri zaidi zitakapotimizwa," aliwaambia waandishi wa habari mjini Kinshasa.

Reuters