Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Jumamosi lilielezea "wasiwasi wake mkubwa" juu ya shambulio linalotishiwa kufanywa dhidi ya al-Fashir katika jimbo la Kaskazini la Darfur nchini Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF).
RSF na washirika wake walivamia miji mikuu minne ya jimbo la Darfur mwaka jana, na walilaumiwa kwa kampeni ya mauaji ya kikabila dhidi ya makundi yasiyo ya Kiarabu na ukiukwaji mwingine katika Darfur Magharibi.
Al-Fashir ni jiji kuu la mwisho katika eneo kubwa la magharibi la Darfur ambalo haliko chini ya udhibiti wa RSF.
Baraza la Usalama, katika taarifa, limeelezea wasiwasi wao mkubwa juu ya mashambulizi ya ghafla ya Vikosi vya Msaada wa Haraka na wanamgambo washirika wao dhidi ya mji wa al-Fashir.
"Tunatoa wito kwa Vikosi vya Wanajeshi vya Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka kukomesha uundaji wa vikosi vya kijeshi na kuchukua hatua za kupunguza hali hiyo," ilisema taarifa hiyo.
Maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa walionya Baraza la Usalama wiki iliyopita kwamba takriban watu 800,000 katika al-Fashir walikuwa katika "hatari kubwa na ya haraka" huku ghasia zinazozidi kuongezeka na kutishia "kuanzisha mapigano ya umwagaji damu kati ya jumuiya kote Darfur."
Vita vilizuka nchini Sudan mwaka mmoja uliopita kati ya jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF, na kusababisha mzozo mkubwa zaidi wa watu kuhama makazi yao.
Eneo la AL Fashir ndilo la pekee limesalia chini ya vikosi vya jeshi la taifa katika eneo hilo na ndio ngome kuu ya usambazaji misaada na pia eneo linalowashikilia wakimbizi wengi.
Umoja wa Mataifa umesema karibu watu milioni 25 - nusu ya wakazi wa Sudan - wanahitaji msaada na wengine milioni nane wamekimbia makazi yao.
Wafadhili wiki iliyopita waliahidi zaidi ya $2bn kwa nchi hiyo iliyokumbwa na vita katika mkutano wa Paris.