Ukosefu wa rasilimali za kutosha, vurugu zinazoendelea katika kanda na majanga ya ndani, kama vile mafuriko ni sehemu tu ya orodha ndefu ya matatizo yanayokabili taifa hilo changa la Afrika Mashariki.
Lakini mtiririko wa hivi majuzi wa wakimbizi kutoka Sudan unaleta tishio kubwa zaidi kwa kukwamisha maendeleo ya mkataba wa amani na makubaliano ya utawala nchini humo.
Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) Nicholas Haysom, alionya baraza la usalama kuwa kuongezeka kwa ghasia katika maeneo ya Malakal kunatishia kuhujumu uwepo wa nafasi ya kiraia na kisiasa kabla ya kufanya uchaguzi wa kuaminika.
"Sasa si wakati wa kusinzia juu ya Sudan Kusini," alisema. ''Wakati wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu wanarekebisha mipango yao ya kukabiliana na mahitaji ya wakimbizi hao, kuna dharura ya ufadhili wa ziada na rasilimali ili kukidhi ongezeko katika mahitaji.'' Aliongeza.
Mtiririko wa wakimbizi
Tangu mwezi wa Aprili, zaidi ya watu 117,000 wamehama kutoka Sudan hadi Sudan Kusini, na hivyo kuathiri hali ya uchumi ambayo tayari ni tete.
Wakati wa mkutano huo maalum siku ya Jumanne, Pedro Comissario, mjumbe kutoka Msumbiji, ambaye pia alikuwa akizungumza kwa niaba ya Gabon na Ghana, alisema kwamba pande zote nchini Sudan Kusini lazima zifanye kazi kwa pamoja ili kutimiza ahadi zao katika mkataba wa amani waliokubaliana.
‘’UNMISS inapaswa kuendelea kuzingatia hatua zinazolinda raia. Ongezeko la wakimbizi, pamoja na kupungua kwa mtiririko wa bidhaa na mafuta kutoka Sudan, kumezidisha hali mbaya ya kibinadamu ambayo tayari ni mbaya.’’ Alisema.
Kuongezeka kwa ghasia za hivi majuzi katika mji wa Malakal kunaongeza mtandao mpana wa migogoro ya kijamii ambayo Sudan Kusini inapambana nayo.
UN inaonya kwamba bila nafasi ya kutosha ya kiraia na kisiasa, hakuna mchakato wa uchaguzi unaoweza kuzingatiwa kuwa wa kuaminika.
Sudan Kusini inapanga kufanya uchaguzi Disemba 2024.