Mashirika ya misaada yameonya kutokea mkasa mkubwa iwapo mkataba wa nafaka wa Bahari Nyeusi utavunjwa.
"Kutofanywa upya kwa mpango wa Bahari Nyeusi kutaathiri vibaya sana Afrika Mashariki," Dominique Ferretti, afisa mwandamizi wa dharura wa mpango wa chakula duniani WFP, aliambia mkutano wa Geneva.
"Kuna idadi ya nchi ambazo zinategemea ngano ya Ukrain na bila hiyo tungeona bei za vyakula za juu zaidi," aliongeza.
Kwa mujibu wa taarifa katika shirika la Reuters, WFP inalenga kuweka hifadhi ya chakula kingi iwezekanavyo na italazimika kutafuta wazalishaji mbadala iwapo makubaliano hayo yatafutiliwa mbali.
Moscow imekuwa ikitishia kuachana na mpango unaojulikana kama mpango wa nafaka wa Bahari Nyeusi - uliosimamiwa na Umoja wa Mataifa na Uturuki Julai mwaka jana - ikiwa vikwazo kwa usafirishaji wake wa nafaka na mbolea havitaondolewa.
Kupitia juhudi za Uturuki, Urusi ilikubali kuongeza muda wa mkataba kwa miezi miwili zaidi mnamo Mei, ambao unamalizika Julai 18, na ndio maana wasiwasi umeongezeka kuwa muda huo usipo ongezwa, basi upitishaji wa nafaka utahujumiwa.
Ukraine na Urusi wote ni wasambazaji wakuu wa kimataifa wa ngano, shayiri, mafuta ya alizeti na bidhaa nyingine za bei nafuu za chakula ambazo mataifa yanayoendelea yanategemea.
Zaidi ya tani milioni 30 za nafaka na vyakula zimesafirishwa kutoka Ukraine tangu Agosti mwaka jana, kulingana na UN.