Pande zinazo zozana ndani ya Sudan zimeshutumiwa kwa kukiuka mkataba wa kusitisha mapigano  / Picha: AFP

Umoja wa Mataifa umeidhinisha kuongeza muda wa shughuli za ujumbe wake wa misaada nchini Sudan (UNITAMIS) hadi Disemba 2023

Katika kikao maalum Ijumaa, rais wa baraza la usalama la umoja huo wa sasa, Lana Zaki Nusseibeh ameelezea kusikitishwa na namna pande zote mbili zinazo zozana nchini humo zimekiuka makubaliano ya kusitisha vita.

‘‘Kupata msaada wa kibinadamu kutaokoa maisha ya wananchi,’’ aliongeza Bi Nusseibeh.

Alisisitiza pia baraza hilo lazima lifanye kila liwezekanalo kuhakikisha kunapatika makubaliano ya kudumu ya kusitisha mapigano.

Kwa upande wake mjumbe wa kudumu wa Urusi katika baraza hilo, Anna Evstigneeva alitahadharisha kuwa kuendelea kwa machafuko nchini Sudan kunatishia usalama wa mataifa jirani.

Alitoa onyo kwa ‘nguvu za nje’ zinazoingilia siasa za ndani za Sudan huku akitoa wito kwa jamii ya kimataifa kujihusisha tu na ajenda ya kuleta amani na upatanishi nchini humo.

Mjumbe wa China Geng Shuang alipongeza hatua za Umoja wa Afrika katika kutafuta maafikiano katika mzozo huo huku akitoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuunga mkono juhudi hizo.

Awali Alhamisi, Marekani ilitangaza kuwawekea vikwazo viongozi wa pande zinazo zozana baada ya vikao vya kutafuta suluhu vilivyoandaliwa mjini Jeddah kuvunjika ghafla.

Pande zote mbili zimekuwa zikilaumiwa kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha vita na kuruhusu misaada ya kibinadamu kupitishwa kwa waathiriwa wa mapigano hayo.

Tangu kuzuka ghasia hizo Aprili, takriban watu 1,800 wameuawa huku wengine milioni mbili wakiachwa bila makao.

TRT Afrika