Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) imepongeza Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, kwa kufanikisha upatinisho kati ya Somalia na Ethiopia.
Katika taarifa yake iliyotolewa Desemba 12, 2024, Mwenyekiti wa AUC Moussa Faki Mahamat, amempongeza Rais Erdogan kwa kujitolea katika mchakato mzima wa kuzipatanisha nchi hizo mbili majirani, kwa njia ya majadiliano.
“Nampongeza Rais Erdogan kwa kuunga mkono jitihada hizi za upatanisho wa Somalia na Ethiopia, wenye manufaa kwa watu wa nchi hizo mbili,” ilisomeka taarifa hiyo.
Uturuki ilifanikisha makubaliano hayo kufuatia mwaka mmoja uliotawaliwa na mahusiano mabaya kati ya nchi hizo kutoka Pembe ya Afrika.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, ambaye alikuwa mwenyeji wa Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud siku ya Jumatano, huku akiiita hatua hiyo kuwa ya ‘kihistoria’.
Mpango wa kuifikia bandari
Uhusiano kati ya Ethiopia na Somalia uliingia dosari mwezi Januari mwaka 2024, baada ya Addis Ababa kukubaliana na eneo lililojitenga la Somaliland.
Katika makubaliano hayo, Somaliland ingetoa eneo la takribani kilomita 20 katika pwani ya bahari nyekundu ili kuiwezesha Ethiopia kuanzisha kambi ya jeshi la majini.
Kwa upande mwingine, eneo la Somaliland lilipewa ahadi ya kutambuliwa na Ethiopia.
Maridhiano yaliyoendeshwa na Uturuki
Mwezi Mei mwaka 2024, Uturuki ilianzisha mchakato wa maridhiano, ambayo yalifikia kikomo siku ya Jumatano kwa pande zote mbili kufikia makubaliano kwa manufaa ya nchi zao.
Katika mkutano ulioandaliwa na Rais Erdogan mjini Ankara, Waziri Mkuu Abiy na Rais Hassan Sheikh walikubaliana kumaliza tofauti zao kwa manufaa ya raia wa nchi hizo mbili, na bara la Afrika kwa ujumla.
Rais Erdogan aliuita mchakato wa Ankara kama hatua muhimu wa kumaliza mgogoro kati ya Ethiopia na Somalia.
"Kwa sasa tunaweza kuvuka hatua hiyo mbaya na kuweka mawazo yetu kwenye mahusiano mapya kati ya Somalia na Ethiopia kwenye wigo wa ushirikiano na amani," alisema Rais Erdogan.