Mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, ameeleza "wasiwasi mkubwa" kuhusu matukio ya Jumanne katika taifa la Afrika Mashariki, Kenya. Takribani watu watano waliuawa na zaidi ya 90 kujeruhiwa wakati wa maandamano ya kupinga ongezeko la kodi mjini Nairobi. Maandamano pia yalishuhudiwa katika sehemu zingine za nchi, ikiwemo Bonde la Ufa, Kenya Mashariki, na Kenya Kati.
"Mwenyekiti anawahimiza wadau wote kutumia utulivu na kuepuka vurugu zaidi. Mwenyekiti pia anawasihi wadau wa kitaifa kujihusisha katika mazungumzo yenye tija kushughulikia masuala yenye utata yaliyosababisha maandamano hayo.
Rais William Ruto alielezea matukio ya awali kama "ya kihaini", akiapa kuchukua hatua za haraka na za makusudi dhidi ya "wafadhili na waandaaji" wa maandamano hayo.
Ruto, ambaye amepanga bajeti kubwa ya shilingi trilioni 3.9 – au dola bilioni 30 za Marekani – kwa mwaka wa fedha 2024/2025, anasema Kenya inahitaji mapato zaidi ili kuepuka kutegemea mikopo kupita kiasi.
Ili kudhibiti maandamano, serikali Jumanne ilipeleka jeshi kusaidia polisi katika operesheni hiyo.