Msemaji wa Jeshi la Uganda amethibitisha kuwa Jeshi la Ulinzi la nchi hiyo (UPDF) limeingia eneo la Bunia, ambalo ni mjii mkuu wa jimbo la Ituri , sehemu muhimu Mashariki mwa DRC.
Brigedia Jenerali Felix Kulayigye aliliambia Shirika la Habari la Anadolu kuwa UPDF inalenga kuwadhibiti ADF ambao wana uhusiano na Daesh ambao wanaendeleza mauaji ya watu katika kanda hiyo.
Jeshi la Uganda, kwa kushirikiana na Jeshi la Ulinzi la DRC (FARDC), limeendelea kukisaka kikundi cha waasi hao ambao wametokea Uganda na kukita kambi katika misitu ya Congo.
Hili linajiri wakati Uganda inajikuta katika lawama ya kuhusika na mgogoro mwa Mashariki mwa DRC.
Licha ya uwepo wa UPDF Mashariki mwa DRC kusaidia majeshi ya serikali dhidi ya ADF, Umoja wa Mataifa unadai kuwa Uganda imehusika na kutoa mafunzo kwa wapiganaji wa M23.
Hata hivyo, madai hayo yamepingwa na serikali ya Uganda.