Kurugenzi ya Udhibiti wa Uraia na Uhamiaji (DCIC) ya Uganda imefichua kuwa njama mpya inatumika na raia wa kigeni wanaoomba usaidizi kutoka kwa Waganda na wanaodai kuwa wazazi wao, ili kujinyakulia pasipoti za Uganda.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani nchini Uganda, Simon Peter Mundeyi, amesema kuwa Waganda wanapokea chini ya Shilingi milioni 2 ili kusaini stakabadhi za uraia kwa yeyote anayesaka pasipoti ya Uganda kupitia njia ya ulaghai.
Mundeyi ameongeza kuwa wamefanikiwa kuwakamata baadhi ya raia wa kigeni na wazazi wao ghushi na kwa sasa wanazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Jinja baada ya kukutwa na vitambulisho vya kitaifa vya Uganda wakijaribu kukwepa mfumo rasmi.
Uganda inasema imewakamata raia hao wa kigeni kutoka Nigeria, Rwanda, Burundi, DRC, Sudan Kusini, na Eritrea huku wakudai kuwa ni wenye asili ya Baganda, Basoga au Bagisu bila kuwa na uwezo wa kusema neno lolote katika lugha hizo.
Aidha, mwezi uliopita, Kurugenzi hiyo ya Uraia na Udhibiti wa Uhamiaji - DCIC ilitwaa zaidi ya vitambulisho 10,000 vya kitaifa kutoka kwa raia wa kigeni.
Wengi wa wale ambao walipokonywa stakabadhi hizo kwa umiliki bandia ni raia kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Nigeria, Eritrea, Rwanda, Somalia, Ethiopia, na Sudan Kusini.