Rais wa Uganda Yoweri MUseveni amewaaga wakuu wa Jeshi la UPDF waliostaafu nchini Uganda katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Entebbe..
Kustaafu kwa Majenerali hao inajiri wiki moja tu baada ya kundi jingine la maofisa waandamizi 93 wa jeshi la Uganda kuaga kikosi kwenye sherehe iliyosimamiwa na Naibu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Kamanda wa Vikosi vya Nchi Kavu, Luteni Jenerali Peter Elwelu kwenye hafla iliyofanyika katika ukumbi wa makao makuu ya wizara huko Mbuya, Kampala.
Aidha, Rais Museveni aliwasifu majenerali wastaafu kwa kulitumikia jeshi kama la UPDF na kuchangia maendeleo na ustawi wa Uganda.
Miongoni mwa majenerali hao walioagwa na Rais Museveni ni aliyekuwa Inspekta Jenerali wa Polisi Kale Kayihura ambaye alizungumza kwa niaba ya majenerali wenzake waliostaafu.
"Kikosi chenye nguvu cha mapinduzi tulichojenga hakikuokoa Uganda tu, bali kwa namna fulani kilichangia hali fulani katika eneo la Maziwa Makuu. Kwa hiyo, nawapongeza sana kwa kuwa katika kikosi hicho tukufu na kutoa mchango wenu ndani yake kwa sababu imetatua matatizo mengi sana kwa watu wetu." Rais Museveni alisema.
Jenerali Kayihura, ambaye alifutiwa mashtaka yake wiki hii, alikuwa akikabiliana na makosa mawili ya kushindwa kulinda vifaa vya vita na kusaidia utekaji nyara na kurejeshwa kwa wakimbizi wa Rwanda na raia wa Uganda nchini Rwanda kati ya miaka ya 2012 na 2016.
Nawapongeza kwa mchango wao wa muda mrefu katika mapambano yetu.
Rais Yoweri Museveni pia ni Kamanda Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF), Museveni aliwashauri maafisa hao wastaafu kuwekeza katika miradi kabambe kama vile kujenga shule na hoteli na kujilindi dhidi ya kutumia vibaya fedha hizo.
"Kustaafu kwao kusichukuliwe kama kupunguziwa kazi bali ni uhamisho kutoka huduma moja hadi nyingine. Zamani walikuwa wanahudumia nchi, lakini sasa wanaweza kujifanyia kazi wenyewe kwa malipo ya kustaafu waliyoyapokea." Alimaliza.
Waziri wa Ulinzi, Jacob Oboth Oboth, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Wilson Mbasu Mbadi, na familia za maafisa hao walihudhuria hafla hiyo.