Nchi inapojitayarisha kwa uchaguzi wa ndani mnamo Machi 31, wapigaji kura milioni 61, wakiwemo watu milioni 1 watakaoshiriki kwa mara ya kwanza, wanajitayarisha kuchagua viongozi wa mikoa kutoka vyama 34 vya kisiasa.
Wapiga kura wa Uturuki wanajiandaa kwa uchaguzi wa ndani uliopangwa Machi 31.
Baraza Kuu la Uchaguzi (YSK) limetangaza majina ya vyama 36 vya kisiasa ambavyo vinastahili kushiriki katika uchaguzi huo.
Baadhi ya vyama vitakayoshiriki kinyang’anyiro hicho ni Chama cha Haki na Maendeleo (AK), Nationalist Movement Party (MHP), Republican People’s Party (CHP), IYI Party, Grand Union Party (BBP), New Welfare Party ( Yeniden Refah), Chama cha DEM, pamoja na Saadet na vyama vya Demokrat.
Matokeo ya uchaguzi katika miji mikuu mitatu ya Uturuki - Istanbul, Ankara na Izmir - ndio matokeo yanayotarajiwa zaidi katika uchaguzi.
Mjini Istanbul, Murat Kurum, mgombea wa mara ya kwanza wa chama tawala cha AK Party, atachuana na Ekrem Imamoglu, meya wa sasa kutoka chama kikuu cha upinzani CHP.
Mjini Ankara, wagombeaji maarufu ni Turgut Altinok wa Chama cha AK na Mansur Yavas wa CHP. Huku mchakato wa Izmir wagombeaji maarufu ni Hamza Dag kutoka Chama cha AK na Cemil Tugay wa CHP.
Zaidi ya wapiga kura wapya milioni moja
Kati ya wapiga kura 61,441,882 wamejiandikisha kupiga kura katika uchaguzi, 1,032,610 ni vijana ambao wanaweza kupiga kura kwa mara ya kwanza, katika zaidi ya vituo 206,000 vya kupigia kura kote nchini.
Uchaguzi ujao utaamua mameya wa majimbo 81, wilaya 973 na vitongoji 390, pamoja na “mukhtar” 50,336. Pia watachagua wajumbe wa mikutano mikuu ya mkoa na mabaraza ya manispaa.
Kila raia wa Uturuki ambaye amefikisha umri wa miaka 18 siku ya uchaguzi, ana haki ya kupiga kura.
Usambazaji wa karatasi zinazowahusu wapiga kura, ulioanza Februari 29, ulipangwa kuwa umekamilika Machi 24. Wapiga kura hawatahitajika kuja na karatasi zao siku ya uchaguzi.
Wapiga kura wanaweza kuangalia tovuti ya YSK, pamoja na tovuti ya serikali ya kielektroniki, au kupitia aplikeshen ya simu ya YSK, au kutumia nambari ya simu ya YSK "444 9 975", ili kujua eneo la sanduku la kura ambapo wamejiandikisha kupiga kura.
Masaa ya Kupiga Kura
Kwa sababu ya hali ya hewa na nyakati za machweo katika mwezi wa Machi, YSK imesogeza saa za kupiga kura saa moja mbele katika mikoa 32 ya mashariki.
Kura katika maeneo ya Adiyaman, Agri, Artvin, Bingol, Bitlis, Diyarbakir, Elazig, Erzincan, Erzurum, Gaziantep, Giresun, Gumushane, Hakkari, Kars, Malatya, Kahramanmaras, Mardin, Mus, Ordu, Rize, Siirt, Sivas, Trabzon, , Sanliurfa, Van, Bayburt, Batman, Sirnak, Ardahan, Igdir, na Kilis, zitakuwa kuanzia moja asubuhi hadi saa kumi jioni.
Katika majimbo mengine, upigaji kura utafanyika kutoka saa mbili asubuhi hadi saa kumi na moja jioni.
Katika majimbo ya mashariki, ambapo saa za kupiga kura ni kutoka saa moja asubuhi hadi saa kumi jioni, kuhesabu kura haiwezi kuanza kabla ya saa kumi. Katika majimbo mengine, haiwezi kuanza kabla ya saa kumi na moja. Hata kama wapiga kura wote walioorodheshwa katika sanduku la kura wamepiga kura zao, masanduku ya kura hayatafunguliwa kabla ya mwisho wa saa za kupiga kura.
Katika miji mikuu, kura za umeya wa mikoa, umeya wa manispaa, uanachama wa baraza la manispaa, na “mukhtars”kura zitahesabiwa na kujumlishwa kwa kufuatana. Kinyume chake, katika majimbo mengine, kura za umeya, uanachama wa baraza la manispaa, uanachama wa baraza la mkoa na “mukhtar” zitahesabiwa na kujumlishwa kwa kufuatana.