John Dramani Mahama atapeperusha bendera ya chama cha National Democratic Congress katika uchaguzi Ghana mwaka 2024 / Photo: Reuters

John Dramani Mahama amepigiwa kura ya kuwa atakaye peperusha bendera ya chama cha National Democratic Congress, katika uchaguzi wa urais wa Ghana wa 2024. Hiki ni chama kikubwa zaidi cha upinzani nchini Ghana.

Mahama mwenye miaka 64, alishinda kwa kura nyingi, akipata 297,603, sawa na asilimia 98.9, ya kura huku mpinzani wake meya wa zamani wa Kumasi, Kojo Bonsu akipata kura 3,181, sawa na asilimia 1.1.

Zaidi ya wajumbe 355,000 wa chama hicho cha NDC walikuwa wamekusanyika siku ya Jumamosi katika vituo 401 vya kupigia kura kote nchini kwa ajili ya kupiga kura.

Aliyekuwa gavana wa benki kuu, Kwabena Duffuor alijiondoa kwenye kura ya mchujo siku ya Ijumaa.

Mahama atakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa rais Nana Akufo-Addo, ambaye ameshindana naye na Akuffo Addo akamshinda mara mbili - mwaka wa 2016 na 2020.

"Ni mwanasiasa ambaye amejaribiwa kisiasa na anakuja na uzoefu mkubwa," Kwame Asah-Asante, mhadhiri wa sayansi ya siasa katika chuo kikuu cha Ghana, aliiambia AFP. Mahama alihudumu kama rais wa Ghana kuanzia tarehe 24 Julai 2012 hadi 7 Januari 2017.

Hapo awali aliwahi kuwa makamu wa rais wa Ghana kuanzia Januari 2009 hadi Julai 2012, na alichukua madaraka kama rais tarehe 24 Julai 2012 kufuatia kifo cha mtangulizi wake John Attah Mills.

Chama tawala cha ‘New Patriotic Party’ kitafanya mchujo wake mwezi Novemba 2023 huku uchaguzi wa urais ukipangwa kufanyika Desemba tarehe 7 mwaka ujao.

Wadadisi wa masuala ya siasa wanatabiri kwamba Mahama katika kampeni yake ya urais, ataweza kukabiliana na mzozo wa kiuchumi unaoikabili nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Ghana, muuzaji mkuu wa kakao nje ya nchi yake inakabiliwa na mzigo mkubwa wa deni la zaidi ya dola milioni 49 kufikia Novemba 2022.

Serikali inatumia zaidi ya nusu ya mapato yake kulipia madeni. Ghana, pamoja na majirani wa pwani ya Afrika Magharibi Benin, Togo na Ivory Coast, pia inajipanga kwa ajili ya kuongezeka kwa migogoro kutoka kwa vita vya wanajihadi katika mipaka ya kaskazini nchini Burkina Faso, ambapo wanamgambo wa Kiislamu wanadhibiti maeneo makubwa ya ardhi.