Uchaguzi wa Afrika Kusini: ANC yajiandaa kugawana madaraka baada ya matokeo

Uchaguzi wa Afrika Kusini: ANC yajiandaa kugawana madaraka baada ya matokeo

Chama tawala wa ANC kimepata asilimia 40 ya kura, tofauti na asilimia 57.5 katika uchaguzi wa mwaka 2019.
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa  amewahi kupinga wazo la nchi hiyo kutengeneza serikali ya muungano / Picha: Wengine

Chama tawala cha ANC kimekusanya asilimia 40 ya kura kutoka katika vituo vyote, kulingana na taarifa iliyochapishwa katika tovuti ya tume ya uchaguzi ya nchi hiyo siku ya Jumamosi.

Kwa sasa, ni dhahiri kuwa chama cha ANC kitakuwa kinamsaka mshirika ili kijihakikishie kura za kutosha za kumteua Rais na hatimaye kuunda serikali.

Chama hicho kimekusanya kura asilimia 40.14 kutoka uchaguzi wa Mei 29, 2024, tofauti na asilimia 57.5 iliyopata kwenye uchaguzi wa mwaka 2019.

Chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance, kimepata asilimia 21.7 wakati uMkhonto we Sizwe (MK), cha Jacob Zuma, kina asilimia 14.8.

Mazungumzo ya serikali ya muungano

Vyama vya siasa vimeanza kuweka misimamo yao kabla ya mazungumzo ya kugawana madaraka.

"Tumekuwa kwenye mazungumzo na kila mtu hata kabla ya uchaguzi," Naibu Katibu Mkuu wa Nomvula Mokonyane aliiambia AFP, akisema kuwa chombo cha maamuzi cha chama hicho kitatoa mwelekeo wake mara baada ya kutangazwa kwa matokeo ya jumla.

"Ni muhimu kwa maamuzi yoyote kufuata misingi ya kanuni."

Wakati matokeo yanatarajiwa mwishoni mwa juma, wanasiasa na wachambuzi wameelekeza mawazo yao kwenye matarajio ya muungano unaoongozwa na ANC.

Chama cha ANC kimetawala demokrasia ya Afrika Kusini kwa kutoa Marais watano, na iwapo Rais Cyril Ramaphosa atabakia madarakani, basi itamlazimu kutafuta washirika kutoka pande zote.

Muungano wa ANC na DA?

Kutakuwa na upinzani ndani ya harakati zake za kuungana na DA iliyoshika nafasi ya pili, chini ya mwanasiasa mweupe John Steenhuisen, ambaye mpango wake wa soko huria wa ubinafsishaji na kukomesha programu za uwezeshaji watu weusi kiuchumi unakinzana na mila za chama tawala.

Makundi yenye itikadi kali za mrengo wa kushoto yanaongozwa na magwiji wa zamani wa ANC kama vile Julius Malema kutoka EFF na Jacob Zuma wa MK.

Chama cha ANC kinasalia na uaminifu wa wapiga kura wengi kwa nafasi yake kuu katika kupindua utawala wa weupe walio wachache na sera zake zinazoendelea za ustawi wa jamii na uwezeshaji watu weusi kiuchumi zinasifiwa na wafuasi kwa kusaidia mamilioni ya familia nyeusi kutoka katika umaskini.

Lakini kwa zaidi ya miongo mitatu ya utawala ambao haujapingwa, uongozi wake umehusishwa katika kashfa nyingi na kubwa za ufisadi, huku uchumi wa bara hilo ulioendelea zaidi kiviwanda ukidorora na takwimu za uhalifu na ukosefu wa ajira zikizidi kukua.

TRT Afrika
Reuters