Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo iko katika hatua za mwisho kuelekea uchaguzi mkuu wa Disemba 20. Uchaguzi huu iwapo utafanyika kwa amani utakuwa wa pili tangu nchi hiyo kujipatia uhuru wake mwaka 1960.
Rais Felix Tshisekedi, anagombea muhula wa pili wa uongozi wa nchi hiyo, ambayo ukubwa wake ni sawa na bara la Magharibi mwa Ulaya. Changamoto kubwa ipo katika uandaaji na usambazaji wa vifaa vya uchaguzi wa nchi nzima.
Mara hii, Tshisekedi anatoana jasho na wagombea wengine 21 katika uchaguzi huo.
DRC pia ni miongoni mwa nchi maskini duniani huku ikiwa na miundombinu mibovu licha ya nchi hiyo kuwa na utajiri wa rasilimali kubwa ikilinganishwa na taifa lolote duniani.
Tume ya uchaguzi CENI mpaka sasa iko katika hatua za mwisho kusambaza vifaa vya kupigia kura katika vituo zaidi ya 175,000 nchi nzima. Ugumu uko zaidi katika maeneo yenye ukosefu wa amani hasa mashariki mwa nchi.
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini DRC anasema, upigaji kura unatarajiwa kwenda vizuri hasa katika maeneo ya mijini ambapo kuna idadi kubwa ya watu, lakini itaweza kuwa vigumu katika maeneo ya vijijini kutokana na ukosefu ya hali ya uslama na miundombinu mibovu.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wiki iliyopita, liliidhinisha ombi la serikali ya DRC, la kutaka vikosi ya Umoja wa Mataifa MONUSCO vilivyomaliza muda wake kusaidia katika usambazaji wa vifaa vya kupigia kura, hasa mashariki mwa nchi ambapo vikosi hivyo vimepelekwa.
Wakati huo huo, baadhi wanadai kwamba huenda sio vituo vyote vya kupiga kura vitafungulia Disemba 20, kutokana na kukosekana kwa vifaa vya kupiga kura, baadhi vinaweza kufunguliwa siku moja au mbili baadae.
Hofu ya machafuko
Katika ripoti iliyochapishwa mwishoni mwa juma, Shirika la Haki za Binadamu (HRW) limetahadharisha uwezekano wa kutokea kwa machafuko, "hali inayohatarisha kufanyika kwa uchaguzi katika baadhi ya maeneo."
Shirika hilo linasema, limeorodhesha visa vya makundi hasimu kukabiliana tangu mwanzoni mwa mwezi Oktoba ambavyo vimesababisha kuwepo kwa "mashambulio, unyanyasaji wa kingono na kifo kimoja."
Kulingana na historia ya machafuko ya DRC, uchaguzi wa mwaka 2018 uliopita salama uliashiria kuwa uchaguzi wa kwanza kufanyika na kupeana hatamu ya uongozi kwa amani.
Matokeo ya uchaguzi yanatarajiwa kutangazwa siku kadhaa baada ya upigaji kura, wadadisi wa mambo wanasema, hicho ndio kitakuwa kipindi nyeti.
Hofu kubwa iliyopo miongoni mwa wagombea wakuu ni iwapo uchaguzi utakuwa wa huru na haki, huku baadhi wakisema, hawatakubali matokeo iwapo kutakuwa na udanganyifu wowote utakaojitokeza.
Wachambuzi wanasema, vurugu zozote zinaweza kutulizwa iwapo matokeo rasmi yatalingana na yale ya waangalizi wa kimataifa.
Wagombea wa vyama vyote, wanatakiwa kutumia vizuri muda wao uliobaki kabla ya saa sita usiku wa Jumatatu ambao ndio mwisho wa kampeni. Siku moja kabla ya kukutana kwenye sanduku la kura. Nani ataibuka kidedea, ni suala la kusubiri na kuona.