Ubalozi wa Uturuki nchini Sudan Kusini Jumanne ulitoa msaada wa vifurushi 183 vya chakula kwa Waislamu walio katika mazingira magumu nchini Sudan Kusini kama sehemu ya misaada iliyotolewa wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Vifurushi hivyo vya vyakula vyenye mafuta ya kupikia, maharage, mchele, sukari na unga wa mahindi vilikabidhiwa kwa Waislamu nchini Sudan Kusini na Ubalozi wa Uturuki kwa uratibu wa shirika la kutoa misaada la Uturuki TIKA (Shirika la Ushirikiano na Uratibu wa Uturuki) na Baraza la Kiislamu la Sudan Kusini.
Balozi wa Uturuki nchini Sudan Kusini, Erdem Mutaf, alisema kuwa msaada huo ni ishara ya uungaji mkono na mshikamano wa taifa la Uturuki na watu wa Sudan Kusini.
"Tuko chini ya shinikizo kubwa la tetemeko la ardhi, tuna maelfu ya wahanga wa tetemeko la ardhi na tunawaunga mkono kama vile ninyi hapa Sudan Kusini," alisema Mutaf wakati wa usambazaji wa misaada katika mji mkuu Juba.
Mutaf aliyashukuru mashirika ya misaada ya Uturuki na mashirika ya maendeleo kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuwafikia watu walio katika mazingira magumu nchini Sudan Kusini.
Alisema kuwa hawatoi chakula tu pia wanasaidia kujenga uwezo, miradi ya maendeleo, mafunzo ya wanawake, mafunzo ya ufundi stadi, matunzo ya watoto na misaada ya majanga nchini Sudan Kusini.
Abdallah Baraj, katibu mkuu wa Baraza la Kiislamu la Sudan Kusini, alisema wamefurahishwa na msaada wa chakula waliopokea kutoka kwa serikali ya Uturuki.
"Tunaishukuru serikali ya Uturuki kwa kuunga mkono Waislamu nchini Sudan Kusini. Chakula hiki kitasaidia wale wanaohitaji chakula," alisema Baraj.
Aliongeza kuwa walionufaika ni pamoja na wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.
Mohammed Maruk, mmoja wa wanufaika, aliishukuru serikali ya Uturuki kwa kuwapa chakula wakati huu mgumu wakati hawana chochote cha kula.
"Licha ya shida, watu wa Uturuki wanakabiliwa na tetemeko ya ardhi, wameamua kutuunga mkono. Tunashukuru.”