Kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, maarufu kama 'Taifa Stars' kimevuna alama moja tu baada ya kucheza michezo miwili kwenye michuano ya AFCON yanayoendelea nchini Ivory Coast./Picha: Wengine 

Bao la lala salama lililofungwa na Patson Daka, kwa kiasi fulani limezamisha matumaini ya Tanzania kusonga mbele kwenye michuano ya AFCON inayoendelea nchini Ivory Coast.

Kulingana na msimamo wa kundi F, Taifa Stars inayonolewa na wazawa Hemed Morocco akisaidiwa na Juma Mgunda, waliochukua nafasi ya Adel Amrouche baada ya kutimuliwa, inashika mkia, ikiwa na alama moja tu baada ya kutoka sare na Zambia katika mchezo wake wa pili.

Timu hiyo itasubiri miujiza au pengine huruma kwenye mchezo wake wa mwisho dhidi ya majirani zao kutoka DRC, ambao wanashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi hilo.

Ili isonge mbele, Tanzania inahitaji kufunga walau magoli manne na kutoruhusu kufungwa bao lolote kwani ‘Taifa Stars’ imeshakubali kuokota mpira mara nne, ndani ya nyavu zake.

Kwa upande mwingine, Tanzania itakuwa inaomba Zambia ipoteze mchezo wake wa mwisho dhidi ya Morocco, ili matumaini ya kusonga mbele yatimie.

Wakati Tanzania inaomba hayo yatokee, matumaini ya Afrika Mashariki yatahamia DRC, ambayo ina alama mbili, ikiwa haijapoteza mchezo wowote kwenye kundi hilo.

Na kama bahati ‘Chui’ hao watakutana na Tanzania kwenye mchezo wao wa mwisho utakaopigwa January 24.

Macho na masikio ya wanaafrika mashariki yatahamia kwenye mchezo huu, tofauti na awali walipoingalia Tanzania kama mwakilishi wa eneo hilo la Afrika Mashariki, hivi sasa, DRC inaangaliwa kwa matumaini makubwa kwamba huenda ikaipeperusha vyema bendera yao.

TRT Afrika