Tanzania imetengaza siku rasmi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Kulingana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohammed Mchengerwa uchaguzi huo umepangwa kufanyika Novemba 27, 2024.
"Kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa za Mwaka 2019, ibara 4 (1-3) (Matangazo ya Serikali Na. 571, 572, 573 na 574) ya mwaka 2024, ninautangazia umma wa watanzania na vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu kuwa tarehe 27 Novemba 2024 itakuwa ni siku ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Tanzania Bara," alisema Mchengerwa.
Mchengerwa alitoa tangazo hilo mjini Dodoma siku ya Agosti 16, ambapo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara 145 na 146 inaelezea uwepo wa Serikali za Mitaa ukilenga kupeleka madaraka kwa wananchi.
Mara ya mwisho kwa Tanzania kufanya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ilikuwa ni Novemba 2019.
Vyama vya siasa 18 kati ya 19 vyenye usajili wa kudumu nchini Tanzania vilihudhuria tukio hilo la kutangazwa tarehe ya uchaguzi huo, huku Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kikishindwa kupeleka mwakilishi.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni hatua muhimu kwa Tanzania, wakati taifa hilo likijiandaa kufanya Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.