Bodi ya Sukari Tanzania (SBT) imetangaza bei mpya kwenye bidhaa ya Sukari nchini humo.
Kulingana na tangazo lilitolewa na bodi hiyo, bei ya jumla kwa maeneo mengi ya nchi hiyo itakuwa kati ya Shilingi za Kitanzania 2,600 had 2,900 wakati kwa upande wa rejareja, bidhaa hiyo itanunulika kwa kiasi cha kuanzia 2,700 had 3,200.
Hatua hii, inafuatia kupanda kwa bei ya sukari hadi kufikia fedha taslimu za Kitanzania 4,000 kwa kilo kutokana na kudimika kwa bidhaa hiyo.
Serikali ya nchi hiyo pia imesema kuwa kiwango cha uzalishaji wa Sukari kimeshuka kwa tani elfu moja kwa siku kutokana na mvua kubwa zinazoendelea nchini humo.
Hivi karibuni, Waziri wa Kilimo nchini Tanzania Hussein Bashe, alibainisha kushuka kwa kiwango cha uzalishaji wa Sukari katika viwanda saba nchini humo, kufuatia mvua za El-Nino, zinazoshuhudiwa maeneo tofauti nchini Tanzania.
Mvua hizo zimeathiri uvunaji wa miwa mashambani na kupunguza kiwango cha sukari katika miwa, kwa zaidi ya asilimia 25.
Kwa mujibu wa Waziri Bashe, mahitaji ya Sukari nchini Tanzania, yanafikia tani 1,500 kwa siku.