Tanzania imepokea vichwa vitano vya umeme na mabehewa yake matatu, ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR).
Seti hiyo ya kwanza ya treni ya EMU, kutoka kampuni ya Hyundai Rotem ya nchini Korea Kusini.
Katika taarifa yake kwa umma, Shirika la Reli Tanzania (TRC), limesema kuwa seti moja ya EMU ina uwezo wa kubeba abiria 589 na kutembea kwa kasi ya kilomita 160 kwa saa.
Chombo hiki kimeundwa kwa mfumo wa teknolojia ya kisasa yenye kumfanya abiria kupata huduma muhimu kama vile intaneti, sehemu za kukaa watu wenye mahitaji maalum na kamera za usalama.
"Hadi sasa, TRC imepokea jumla ya mabehewa 65 ya abiria, vichwa tisa vya umeme na seti moja ya EMU," imesomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa TRC, seti nyengine za EMU zitaendelea kuwasili kila mwezi hadi ifikapo Oktoba 2024.
Mradi huo, unatarajiwa kuanza rasmi mwezi Julai mwaka huu. Awamu ya kwanza ya mradi huo, inatarajiwa kuanza kati ya jiji la biashara la Dar es Salaam hadi Mkoa wa Morogoro, na hatimae awamu nyengine kufuatia.
Mapema wiki hii, Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa alipokuwa Bungeni akielezea utekelezaji wa miradi nane ya kielelezo kwa mwaka 2023/2024, amesema serikali tayari ishatumia kiasi cha shilingi trilioni 10.69 kwa ajili ya ujenzi wa SGR yenye urefu wa kilomita 1,219 kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.
Aidha ameongeza kusema kuwa tayari reli hiyo imeshaanza kufanyiwa majaribio kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro.
“Kama nyote mlivyoshuhudia, majaribio ya treni hiyo ya mwendo kasi yalifanyika kwa mafanikio makubwa mwezi Februari, 2024. Ni matarajio yetu kuwa huduma ya usafiri na usafirishaji itaanza ifikapo Julai, 2024 kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Dodoma,” amesema Waziri Mkuu.