Wakati kampuni hiyo kubwa kutoka Ujerumani inakiri na kuwa tayari kulipa kiasi hicho, Taasisi ya Kuzuia na Kupambambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) imesema inafuatilia kwa ukaribu maendeleo ya sakata hilo.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Kamishna Salum Hamduni, tayari mamlaka za juu nchini Tanzania ikiwemo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na ofisi ya Mwanasheria Mkuu, wanalipa uzito suala hilo.
Kamishna Hamduni alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini Tanzania kuwa mamlaka hizo zilikuwa zinasubiria nyaraka muhimu kutoka mamlaka za Marekani.
Katika sakata hilo, maafisa kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), wanatuhumiwa kupokea Dola za Kimarekani 800,000 kama hongo ili kuipa zabuni yenye thamani ya takribani Dola za Kimarekani bilioni 6.6 iliyohusisha kutoa leseni na huduma za programu kwa mwaka 2014/15.
Inadaiwa kuwa, maafisa hao walipokea pesa hizo kwa awamu mbili.
Hata hivyo, kampuni hiyo kutoka nchini Ujerumani ilishindwa kutimiza masharti ya mkataba huo na kuilazimu Tanzania kubatilisha makubaliano hayo ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria maafisa waliohusika.
Mbali na Tanzania, nchi vyengine zinazotuhumiwa kuhusika na mtandao wa rushwa kutoka kampuni ya SAP ni pamoja na Azerbaijan, Ghana, Indonesia, Malawi, Kenya na Afrika ya Kusini.