Tanzania inakuwa kuwa miongoni mwa nchi 7 barani Afrika zinazotoa huduma ya upandikizaji uloto

Na Lulu Sanga

Tanzania imetangaza rasmi kuwa imefanikiwa kwa mara ya kwanza kupandikiza uloto yaani 'Bonmarrow' katika hospitali yake iliyopo katika makao makuu ya nchi hiyo jijini Dodoma

Kwa mujibu wa taarifa ya nchi hiyo, huduma hii mpya itasaidia kutibu ugonjwa wa Selimundu (Sickle Cell) huku mpaka sasa wagonjwa 3 wakiwa wametibiwa na kupona.

Katika ufafanuzi wake, Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya Benjamin Mkapa, Dkt. Alphonce Chandika anasema kwamba tangu Januari 19, mwaka huu hadi leo, wamefanikiwa kupandikiza uloto kwa watoto watatu na wote wanaendelea vizuri

"Kwa awamu hii ya kwanza tumefanikiwa kupandikiza watoto 3 ambao wanaendelea vizuri kiafya na leo wataruhusiwa kwenda nyumbani" Dkt Chandika Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma anaeleza

Huduma ya upandikizaji uloto Tanzania imezinduliwa na Waziri mkuu wa nchi hiyo Kassim Majaliwa ambaye anasisitiza ni ushahidi tosha wa namna ambavyo Tanzania inapiga hatua kuboresha huduma za afya • Text

“Huduma za namna hii kuendelea kutolewa katika hospitali zetu si jambo dogo, na hasa kwa kuzingatia ukweli kuwa huduma kama hizi zinapatikana katika nchi chache sana kwenye bara la Afrika.”

Kufanyika upandikizaji wa uloto nchini humo, kumeifanya Tanzania iwe miongoni mwa nchi saba zinazotoa huduma hiyo barani Afrika.

Nchi nyingine zinazotoa huduma ya upandikizaji uloto barani Afrika ni Algeria, Afrika ya Kusini, Misri, Morocco, Nigeria na Tunisia.

Hii inamaanisha kuwa Tanzania inakuwa nchi ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kuanza kutoa huduma hii.

TRT Afrika