Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi wa Tanzania, Hamad Masauni amekutana na viongozi wa Jeshi la polisi nchini humo kujadili hali ya usalama na amani ya nchi.
Kikao hicho, kilichofanyika jijini Dodoma, pia kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya ndani wa nchi hiyo, Daniel Sillo, kiliangazia hali ya amani na usalama ikiwemo matukio ya uhalifu yanayotokea nchini humo na hatua zilizochukuliwa.
Hatua hiyo inakuja wakati Tanzania ikishuhudia ongezeko la matukio ya kihalifu katika siku za hivi karibuni, ikiwemo kupotea kwa watu, ubakaji, utekwaji na mauaji.
Kikao hicho, pia kinakuja wakati makundi mbalimbali yakiwemo Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kupaza sauti dhidi ya vitendo hivyo, na kuitaka serikali ya nchi hiyo kuchukua hatua za haraka kudhibiti vitendo hivyo.
Baadhi ya wadau hao ikiwemo vyama vya siasa wamewatupia lawama Jeshi la Polisi wakiwashtumu kuhusika na baadhi ya vitendo, jambo ambalo Polisi wamelikanusha.