Rais wa Tanzania anaamini kuwa katika kipindi cha miaka 60, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limehakikisha ulinzi wa mipaka na kuwa kimbilio la wananchi na kuwa mstari wa meble pindi wananchi wanapokabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo majanga asili au ajali.
Kulingana na kiongozi huyo, Jeshi hilo limetimiza wajibu na majukumu yake kikamilifu kwa ujasiri, uhodari na ufanisi mkubwa na hivyo kuendelea kuwa Jeshi la ulinzi, ukombozi na kioo katika harakati za ukombozi wa Afrika na kulinda amani ya dunia.
Rais Samia amesema hayo wakati wa maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa JWTZ.
Jeshi hilo lilianzishwa rasmi Septemba 1, 1964 likiwa na lengo la kulinda uhuru wa nchi na mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“JWTZ imekuwa kinara katika kutafsiri Dira, Sera na Mipango ya Serikali katika awamu zote za uongozi, na pia limegusa maisha ya wananchi kwa kutoa huduma za kijamii kama afya na elimu kwa kuendesha hospitali na shule kwa ambazo zinahudumia wanajeshi na raia,” amesema Rais Samia katika taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu ya nchini Tanzania.
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu aliongoza maadhimisho hayo yaliyofanyika katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.
Mara baada ya kuanzishwa kwake, JWTZ ilikuwa na dira ya kuwa na jeshi dogo, shupavu la viongozi na wataalamu wenye zana na silaha za kisasa, utayari wa hali ya juu katika Ulinzi wa nchi ya Tanzania.
Vilevile, ilikuwa na dhima ya kulinda nchi na kutetea maslahi ya Taifa la Tanzania, kutoa msaada kwa mamlaka za kiraia na kuwezesha kufikiwa kwa malengo ya kitaifa na kimataifa.