Kupitia taarifa kutoka Ikulu ya Tanzania rais Samia amesema hayo leo akiwa na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Indonesia Joko Widodo aliyepo nchini kwa ziara ya kiserikali ya siku mbili wakati wakizungumza na vyombo vya habari.
Aidha, Rais Samia amesema kituo hicho kilichoanzishwa mwaka 1996 na Serikali ya Indonesia kimechangia kwa kiasi kikubwa kuelimisha wakulima na kutoa mafunzo kwa wataalam wa kilimo.
Rais Samia pia amesema Tanzania na Indonesia zimekubaliana kukuza biashara na uwekezaji kwa kuzileta pamoja sekta za umma na binafsi ili kuimarisha ushirikiano katika viwanda, kilimo, nishati, madini, mafuta na gesi, uvuvi na utalii.
Vile vile, Rais Samia amesema majadiliano yao yamebainisha nia ya Tanzania kupata uzoefu wa uzalishaji mafuta kutoka kwa Indonesia ambaye ni mzalishaji mkubwa zaidi wa mafuta ya mawese duniani.
Hali kadhalika, Rais Samia amesema Serikali ya Tanzania imejidhatiti kuhakikisha inaongeza uzalishaji wa mafuta ya kula ili iache kabisa kutumia fedha zake za kigeni kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi.
Nchi hizo mbili zimetiliana saini hati 7 za Makubaliano (MoUs) ikiwemo sekta za ulinzi, nishati, kilimo, mifugo, uvuvi na uchumi wa buluu, madini, na pia misamaha ya viza kwa wamiliki wa hati za kusafiria za kidiplomasia na za huduma.