Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akishuhudia Utiaji Saini wa Mikataba Mitatu ya msaada uliotolewa na Umoja wa Ulaya yenye thamani ya Euro Milioni 179.35 sawa na Shilingi Bilioni 455.09 za Kitanzania na kupewa Msaada wa Bajeti ya Serikali kiasi cha Euro Milioni 46.11 sawa na Shilingi Bilioni 117.036 za Kitanzania kwa waka wa Fedha 2022/2023 kutoka Umoja wa Ulaya. Mikataba hiyo imetiwa Saini na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Natu El-maamry Mwamba na Balozi wa Umoja wa Ulaya hapa Nchini Mhe. Manfredo Fantl katika Ukumbi wa Hazina Mkoani Dodoma 04 Julai, 2023. Picha: Ikulu Tanzania

Utiaji saini huo ulifanyika katika Ukumbi wa Hazina Mkoani Dodoma ukishuhudiwa na Rais Samia Suluhu Hassan huku hiyo Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Natu El-maamry Mwamba na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania Manfredo Fantl.

Fedha hizo zinajumuisha msaada wa Bajeti ya Serikali kiasi cha Euro Milioni 46.11 kupiga jeki bajeti ya mwaka wa Fedha 2022/2023.

Kulingana na taarifa rasmi kutoka msemaji wa Ikulu Tanzania, Zuhura Yunus, miongoni mwa sekta zitakazonufaika na fedha hizo ni uchumi wa bluu, uwezeshaji wananchi kiuchumi, pamoja na uimarishaji mifumo ya ukusanyaji na usimamizi wa fedha serikalini.

Haya yanajiri kufuatia mkutano kati ya Rais Samia Suluhu na Rais wa tume ya Ulaya Ursula Von Der Leyen uliofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Ulaya, mapema mwaka uliopita.

TRT Afrika na mashirika ya habari