Opposition leader Tundu Lissu to return from exile after the lifting of a ban on political rallies / Photo: AFP

Mmoja wa viongozi wakuu wa upinzani nchini Tanzania na aliyekuwa mgombea urais Tundu Lissu ameachiwa kwa dhamana mapema Jumatatu, tarehe 11 Septemba, saa chache baada ya kuzuiliwa na polisi kwa madai ya kufanya mkusanyiko usio halali.

Lissu amekwaruzana na vyombo vya usalama tangu aliporudi nchini Tanzania kutoka uhamishoni nchini Ubelgiji.

Kiongozi huyo wa upinzani, ambaye pia ni naibu mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani Tanzania CHADEMA, anadaiwa kufanya mikutano ya kisiasa sehemu mbali mbali nchini Tanzania tangu kurudi kwake, ambapo amekuwa akikashifu hadharani uongozi wa Rais Samia Suluhu na hasa hivi majuzi amekosoa mkataba wa kubinafsisha bandari na makubaliano kati ya nchi na shirika kutoka UAE ya DP World.

Hata hivyo taarifa ya polisi ilisema kuwa Lissu alikamatwa kwa kosa la kufanya mikutano bila idhini.

"Lissu yuko chini ya ulinzi pamoja na watuhumiwa wengine watatu kwa kosa la kuitisha mikutano isiyo halali na kuzuia maafisa wa sheria kufanya kazi zao," Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo alisema katika taarifa yake Jumapili.

Baada ya kuachiliwa, Lissu alizungumza na waandishi wa habari akidai kuwa kukamatwa kwake kunahusiana na malalamiko yake juu ya kuhamishwa kwa jamii ya Wamaasai kutoka hifadhi ya Ngorongoro.

TRT Afrika