Kampuni ya Ndege ya Tanzania inatarajiwa kupokea ndege mpya aina ya Boeing B787-8 Dreamliner, yenye uwezo wa kubeba abiria 262.
Tukio la mapokezi ya ndege hiyo mpya linatarajiwa kufanyika siku ya Agosti 19, katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume, Zanzibar.
Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania, Makame Mbarawa amesema kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Hussein Ali Mwinyi atashiriki kuipokea ndege hiyo.
Aidha, Profesa Mbarawa amesema kuwa ndege hiyo, ambayo ni ya tatu katika familia ya Boeing B787-8, ina uwezo wa kubeba abiria 262 ambapo viti 22 ni vya daraja la biashara na viti 240 ni daraja la kawaida.
"Pia, ndege hii ina uwezo wa kubeba mizigo kati ya tani 15 hadi 20 kulingana na ujazo wa abiria na mizigo yao," ameeleza Waziri huyo.
Manunuzi ya ndege
Mwaka 2016, Serikali ya Tanzania ilichukua hatua mbalimbali za kuifufua ATCL, ikiwemo ununuzi wa ndege mpya, kufanya mabadiliko ya Menejimenti na Bodi ya Wakurugenzi na kuipatia mtaji wa kibiashara.
Hadi kufikia Disemba, 2023 ATCL imeshapokea ndege mpya 14 ambazo zimenunuliwa na Serikali.
Ndege hizo ni pamoja na mbili za masafa marefu aina ya Boeing 787-8 Dreamliner zenye uwezo wa kubeba abiria 262 kila moja; ndege mbili (2) aina ya Boeing 737-9 Max yenye uwezo wa kubeba abiria 181, ndege nne (4) za masafa ya kati aina ya Airbus A220-300 zenye uwezo wa kubeba abiria 132 kila moja; ndege tano (5) za masafa mafupi aina ya Dash 8 Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja na ndege kubwa ya mizigo aina ya Boeing 767-300F yenye uwezo wa kubeba tani 54.
"Kupokelewa kwa ndege hii mpya ya masafa marefu kunaiwezesha ATCL kuwa na jumla ya ndege 16 ambapo ndege 15 ni mpya ambazo zimenunuliwa kutokana na mpango wa ufufuaji wa ATCL ulioanza kutekelezwa mwaka 2016 na ndege moja ya zamani," aliongeza Profesa Mbarawa.
Kulingana na Waziri huyo wa Uchukuzi wa Tanzania, ujio wa ndege hiyo utaiwezesha kampuni ya ATCL kuongeza miruko ya safari zake kwa vituo vya Kikanda na Kimataifa ambavyo wanahudumia kwa sasa pamoja na kuanzisha safari mpya za Kinshasa, Goma, Muscat na Lagos.
Pamoja na faida za moja kwa moja kibiashara, ujia wa ndege hiyo pia utaongeza pia fursa za ajira kwa Watanzania, na kukua kwa Sekta ya Utalii.