Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeanza mchakato wa kulipa fidia kwa wakazi waliopisha mradi wa ujenzi wa reli ya kiwango cha kisasa (SGR), ambao ujenzi wake unahusisha eneo la Isaka na Mwanza.
Malipo hayo yanahusisha wakazi ambao makaburi a ndugu zao yalihamishwa ili kupisha ujenzi wa reli hiyo yenye urefu wa kilomita 341.
Kulingana na afisa mazingira wa TRC Nelly Mleleu, shirika hilo limeanza malipo kwa wakazi wa miko ya Tabora, Shinyanga, Simiyu, na Mwanza, ambao iliwalazimu wahame ili kupisha ujenzi wa reli hiyo ambao utagharimu Dola Bilioni 1.3.
“Tunafurahia ushirikiano tulioupata kutoka kwa viongozi vya vijiji husika ambavyo mradi huu unapita, na TRC itahakikisha kuwa mchakato huo unaendelea vizuri kwa kuzingatia ulinzi wa mazingira na usalama wa wakazi,” alisema Mleleu.
Mradi huo unaotekelezwa kwa muda wa miezi 36 unatekelezwa na kampuni ya China Civil Engineering Construction (CCEC), na China Railway Construction Corporation (CRCC).
Pia unahusisha madaraja makubwa 43, vivuko vya chini 44, vya juu 23 na makalvati 591 na daraja refu eneo la kuingia Mwanza, vituo 9, stesheni kubwa ya Mwanza na pia kutakuwa na karakana kubwa eneo la Fela na Tabora kwa ajili ya reli hiyo.