Magari ya MwendoKasi Dar es Salaam| Picha: TRT Afrika

Serikali jana ilitoa ruhusa rasmi kwa mabasi ya abiria kwenda vijijini kufanya kazi kwa masaa 24 kwa lengo la kuchochea zaidi uchumi katika sekta ya usafirishaji.

"Tumefurahi sana, na tunamshukuru Waziri Mkuu maana hii kitu yakufanya kazi masaa marefu ilikuwa inavuruga mipango, sasa tutaokoa muda." Asema Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania, TABOA, Priscus Joseph katika maongezi na TRT Afrika leo.

Tangazo hilo linafuta marufuku iliyowekwa katika miaka ya 1990 na linajibu mahitaji ya muda mrefu ya baadhi ya wamiliki na madereva wa mabasi ambao walitaka operesheni ifanyike kwa masaa 24 kama ilivyo katika nchi nyingine.

Uamuzi huu mpya, kwa mujibu wa serikali, unakuja baada ya mabadiliko chanya katika miundombinu, usalama kupitia doria za polisi na kuzingatia maoni ya wadau mbalimbali katika sekta ya usafirishaji.

Waziri Mkuu alikuwa akizungumza wakati wa kufunga kikao cha 11 cha bunge la 12 Dodoma, akibainisha kwamba marufuku ya mwaka 1990 ilisababishwa na matukio ya utekaji nyara wa mabasi ambayo yalisababisha uporaji na unyanyasaji wa abiria.

Sababu nyingine, alisema, ni ajali mbaya za mabasi ambazo zilisababisha vifo vya watu na kupelekea baadhi kupata ulemavu wa kudumu na uharibifu wa mali na miundombinu ya barabara. Utekaji nyara wa mabasi, alibainisha, ulikuwa ukifanyika katika maeneo yenye barabara mbovu na mtandao duni wa mawasiliano.

"Mtu sasa anapanda gari asubuhi kwa mfano kutoka Mbeya kwenda Dar na anarudi siku hio hio kupunguza gharama akishamaliza kufunga mzigo wake." Asema Priscus Joseph akiongeza kuwa magari na ushindani ya kijinga pia unapungua, yani magari ambayo yalikuwa yanashindana wakijua wana safari moja tu siku nzima sasa hawa presha.

Baada ya hatua zilizochukuliwa kupunguza kwa kiasi kikubwa au kuondoa kabisa changamoto za usalama na miundombinu iliyokuwepo wakati huo, serikali haikuwa na chaguo lingine ila kuruhusu usafirishaji kufanya kazi mchana na usiku.

Pia ilikuwa imepita na wakati, ukiangalia katika EAC, Kenya, Rwanda, Uganda wote wanatembea usiku. Kwanini hatutembei usiku? Haina tija!

Priscus Joseph, Katibu Mkuu TABOA

"Siku hizi watu hawaibiwi kijinga maana hawabebi hela mkononi kwa hio swala la usalama limeongezeka maradufu, biashara zitaongezeka na nchi itapata tija na ishu nzuri ya kimaendeleo".

TRT Afrika