Likiwa limeanzishwa miaka 27 iliyopita, chimbuko la ZIFF ni kwenye kisiwa cha Unguja, huko Zanzibar ambapo ndiko lilikosajiliwa; na kulifanya kuwa tamasha kubwa na kongwe zaidi la filamu, kusini mwa jangwa la Sahara./Picha: ZIFF    

Na Edward Qorro

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Bila shaka, Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF) si geni masikioni mwa Waafrika.

Likiwa limeanzishwa miaka 27 iliyopita, chimbuko la ZIFF ni kwenye kisiwa cha Unguja, huko Zanzibar ambapo ndiko lilikosajiliwa; na kulifanya kuwa tamasha kubwa na kongwe zaidi la filamu, kusini mwa jangwa la Sahara.

Wakati Zanzibar inaendelea kuwa moja ya kivutio kikubwa cha utalii duniani, kutokana na utajiri wa historia yake, tamasha la ZIFF pia limechangia kuongeza nakshi kwenye historia hii.

“Kuendeshwa kwa tamasha kwa kipindi cha miaka 27 ni mafanikio tosha, na ZIFF imeendelea kuutangaza utamaduni wa taifa la Tanzania kote ulimwenguni kupitia utazamaji wa filamu,” Mkurugenzi wa ZIFF Hatibu Madudu, anaiambia TRT Afrika katika mahojiano maalumu.

Wakati Zanzibar inaendelea kuwa moja ya kivutio kikubwa cha utalii duniani kutokana na utajiri wa historia yake, tamasha la ZIFF pia limechangia kuongeza nakshi kwenye historia hii./Picha: ZIFF

Kulingana na Madudu, tamasha la ZIFF limekuwa kitovu cha mafunzo kwa watengeneza filamu wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla na ndio chimbuko la tamasha kubwa la muziki la Sauti za Busara.

“Na ndio maana tumeendelea kutoa tuzo kwenye vipengele tofauti kama vile Filamu Bora Ndefu hapa Afrika Mashariki, Mwigizaji Bora wa kike na kiume Tanzania, Mwigizaji bora wa kike na kiume Afrika Mashariki, Filamu bora fupi, Filamu bora katika tuzo maalum ya Osmane Sembene ya maendeleo ya Afrika, Filamu bora Makala, Filamu bora kutoka visiwani Zanzibar inayotolewa kwa ushirikiano na taasisi ya Emerson pamoja na Tuzo ya maisha,” Madudu anaeleza.

Tamasha hilo, ambalo kwa mwaka huu litafanyika kuanzia Agosti 1 mpaka 4, pia limeendelea kusheheni burudani tofauti kama vile uoneshwaji wa filamu za wanawake, watoto, mafunzo na warsha, mijadala, na michezo ya mbio za ngalawa na majahazi, soka bila kusahau burudani na muziki.

Mkurugenzi wa ZIFF, Hatibu Madudu(kushoto) akifurahia jambo na mkufunzi wa filamu barani Afrika, Profesa Martin Mhando./Picha: ZIFF

Pia hutoa fursa ya kipekee kwa wasanii kuhudhuria kujifunza na kukutana na waigizaji na wasanii nguli kutoka nchi za nje.

Kwa mfano, mwaka 2009 Danny Glover ambaye ni mwigizaji maarufu duniani kutoka Marekani, alikuwa ni mmoja wa watu waliohudhuria tamasha hilo kubwa.

Miaka mawili baadae, mwanamuziki nyota wa miondoko ya reggae Orville Richard Burrell CD, maarufu kama Shaggy alikonga nyoyo za watu wengi katika jukwaa la ZIFF.

Msanii Shaggy kutoka nchini Marekani akitumbuiza katika tamasha la ZIFF mwaka 2011./Picha: ZIFF

Kwa namna ya kipekee, tamasha la ZIFF huwapa wasanii furza nzuri ya kujitanua kimataifa kwani wanaweza kupata nafasi ya kujuana na waandaaji wa kimataifa.

Kila mwaka, uongozi wa ZIFF hupokea maelfu ya maombi ya wadau wa filamu kutoka kila kona duniani, wakitaka kupata nafasi ya kuhudhuria kwa kutambua manufaa ya tamasha hilo.

Aliyekuwa msanii maarufu wa filamu nchini Tanzania, Steven Kanumba alitumia vizuri tamasha la ZIFF kumkutanisha na wasanii na watengezaji wakubwa wa filamu duniani.

Tamasha hilo, ambalo kwa mwaka huu litafanyika kuanzia Agosti 1 mpaka 4, pia limeendelea kusheheni burudani tofauti kama vile uoneshwaji wa filamu za wanawake, watoto, mafunzo na warsha, mijadala, na michezo ya mbio za ngalawa na majahazi, soka bila kusahau burudani na muziki./Picha: ZIFF

Hata hivyo, tamasha hilo bado linakabiliwa na changamoto kadhaa, hususan ya ufadhili, hasa kuwezesha kuendesha program za tamasha pamoja na tiketi za ndege na malazi kwa watengeneza filamu, majaji na wakufunzi, wakati wote wa ZIFF.

“Pamoja na ukubwa wake barani Afrika, ZIFF imeendelea kupitia changamoto mbalimbali, lakini bado tunaendelea kusukuma gurudumu,” Madudu anajinasibu.

“Tunaomba wafadhili wajitokeze kwa wingi kutuunga mkono ili nao waweze kufaidika na jukwaa hili kongwe lililoweza kusimama imara na kuaminiwa kwa miaka 27 sasa.”

Tuzo mbalimbali hutolewa kwa waliofanya vizuri wakati wa tamasha hilo./Picha: ZIFF

Kulingana na Madudu, upo mpango wa kufungua wigo mpya wa soko la filamu hususan tamthilia zinazozalishwa katika nchi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, hasa kutokana na ufuatiliaji mkubwa wa tamthilia za kimataifa zilizotafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili.

Mbio za ngalawa na majahazi ni sehemu ya burudani ya ZIFF./Picha:ZIFF

“Nia yangu ni kufanya ZIFF kuwa kituo cha kuwakutanisha wazalishaji na wauzaji na wanunuzi wa tamthilia za lugha ya kiswahili katika ukanda huu kama sio Afrika kwa ujumla,” anasema.

Hata hivyo, tamasha hilo bado linakabiliwa na changamoto kadhaa, hususan ya ufadhili, hasa kuwezesha kuendesha program za tamasha pamoja na tiketi za ndege na malazi kwa watengeneza filamu, majaji na wakufunzi, wakati wote wa ZIFF./Picha:ZIFF

Mkurugenzi huyo wa ZIFF anaweka wazi nia ya kuongeza ushirikiano na matamasha mengine makubwa katika kutanua wigo wake pamoja na kuimarisha na kuboresha warsha na mafunzo kwa watengeneza filamu kwenye ukanda wa Afrika Mashariki.

Shamrashamra za ufukweni kwenye tamasha la ZIFF./Picha: ZIFF

Tamasha la ZIFF lilianzishwa mwaka 1997 kwa nia ya kuendeleza na kukuza tasnia ya filamu na mambo mengine ya kiutamaduni kama kichocheo cha ukuaji wa kijamii na kiuchumi wa kikanda.

Sehemu maarufu ya kuoneshea filamu wakati wa tamsha la ZIFF visiwani Zanzibar, Tanzania./Picha: ZIFF
TRT Afrika