Na Emmanuel Onyango
Swala adimu waliokuwa wamehifadhiwa kwenye mabanda huko nchini Marekani kwa miongo kadhaa, wamerudishwa nyumbani.
Swala hao, maarufu kama Mountain bongo ni moja wa viumbe walioko hatarnini kutoweka, huku wakiwa wanapatikana katika eneo la kati nchini Kenya.
Wakiwa na maumbile makubwa, swala hao walijulikana zaidi kwa mistari meupe kwenye miili yao.
Wengi wao walihamishiwa nchini Marekani kutoka Kenya kwenye miaka ya 60, kupitia mkakati wa serikali ya kikoloni ya Uingereza.
Baadhi ya swala hao walihamishiwa barani Ulaya.

Baadhi ya wanyama wanaorudishwa nchini Kenya ni sehemu ya vichipukizi vya wale walipelekwa nchini Marekani. Wahifadhi wanaamini kuwa hatua hiyo ni ya umuhimu katika kulinda na kuhifadhi wanyama hao.
“Hii ni hatua nzuri kwani hatukuwa tumebakiwa na swala wowote wa aina hiyo hapa kwenye asili yao,” msemaji wa Shirika la Huduma ya Wanyamapori nchini Kenya (KWS) Paul Udoto anaiambia TRT Afrika.
“Washirika wetu wa nchini Marekani wamejaribu kutusaidia kuwarejesha nyumbani.”
Awamu ya kwanza ya wanyama hao 17 iliwasili nchini Kenya siku ya Jumapili kutoka kituo cha kuhifadhia wanyama cha RSCF.
Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Kenya kuongeza idadi ya wanyama hao huku wakiwa wamelenga kutenga eneo la Marania na Mucheene kwenye kaunti ya Meru kama eneo ambalo watafikia wanyamapori hao.

“Ndani ya miezi mitatu ijayo, tutazungumza na wenzetu kutoka Ulaya ili kuleta mbegu za kupandikiza wanyama hao wakiwa hapa,” alisema.
“Tuna uhakika wa kuwahifadhi wanyama hao vyovyote iwezekanavyo," aliongeza.
Wanyama hao watawekwa kwenye eneo maalumu kwa angalau miezi mitatu ili waweze kuzoea mazingira yao mapya.
Kulingana na Waziri wa Utalii wa Kenya Rebecca Miano, wanyama hao wameteseka vya kutosha kwa kipindi cha miongo kadhaa.

Kulingana na Waziri wa Utalii wa Kenya Rebecca Miano, wanyama hao wameteseka vya kutosha kwa kipindi cha miongo kadhaa.
“Walipoteza maeneo yao ya malisho na wengi wao kuwindwa na hivyo idadi yao kupungua maradufu,” alisema.