Mkuu wa majeshi la Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan ameapa kurejesha maeneo zaidi kutoka kwa wapiganaji wa kikosi cha RSF. / Picha: TRT Arabi

Kuundwa kwa serikali mpya ya Sudan kunatazamiwa wakati wowote baada ya kukamilika kwa udhibiti wa mji wa Khartoum, vyanzo vya kijeshi viliiambia Reuters siku ya Jumapili, siku moja baada ya mkuu wa majeshi Abdel Fattah al-Burhan kusema kuwa ataunda serikali ya wataalamu kipindi cha vita.

Jeshi la Sudan, kwa muda mrefu katika vita vyake na wapiganaji wa RSF, katika wiki za hivi karibuni wamerejea katika mji mkuu wa Khartoum na maeneo mengine, na kukaribia ikulu ya rais karibu na mto Nile.

RSF, ambayo imesema ingeunga mkono uundaji wa utawala hasimu wa kiraia, imerudi nyuma, ikizidiwa nguvu na uwezo wa jeshi la anga na wanajeshi wa ardhini wakiungwa mkono na wanamgambo washirika.

"Tunaweza kuiita serikali ya muda, serikali ya wakati wa vita, ni serikali ambayo itatusaidia kukamilisha malengo yetu ya kijeshi yaliyobakia, ambayo ni kuikomboa Sudan kutoka kwa waasi hawa," Burhan aliuambia mkutano wa wanasiasa wanaounga mkono jeshi katika ngome ya jeshi huko Port Sudan siku ya Jumamosi.

Usitishaji vita wa Ramadhani umekataliwa

RSF inadhibiti sehemu kubwa ya magharibi mwa nchi, na inashiriki katika kampeni kali ya kuimarisha udhibiti wake wa eneo la Darfur kwa kuuteka mji wa al-Fashir.

Burhan aliondoa usitishaji vita wa Ramadhani hadi pale RSF itakapositisha harakati zake.

Vita hivyo vilizuka mwezi Aprili 2023 kutokana na mizozo kuhusu kuunganishwa kwa vikosi hivyo viwili baada ya kufanya kazi pamoja kuwatimua raia ambao walikuwa wameunda serikali ya pamoja baada ya vuguvugu lililomuondoa madarakani Omar al-Bashir.

Mzozo huo umesababisha moja ya hali mbaya zaidi kwa raia duniani huku watu zaidi ya milioni 12 wakihama makazi na nusu ya watu wakikabiliwa na njaa.

Mabadiliko ya katiba ya muda

Burhan alisema kutakuwa na mabadiliko katika katiba ya muda ya nchi, ambayo vyanzo vya kijeshi vilisema yataondoa masuala yote ya ushirikiano na raia au RSF, na jeshi litakuwa na mamlaka pekee na kumteua Waziri Mkuu atakayekuwa mtaalamu na atakayeteua Baraza la Mawaziri.

Burhan alitoa wito kwa wanachama wa muungano wa kiraia wa Taqadum kujitenga na RSF, akisema wataruhusiwa kushirikiana nao iwapo watafanya hivyo.

TRT Afrika