Sudan Kusini imethibitisha mlipuko wa ugonjwa wa Mpox, baada ya mtu mmoja kugundulika na virusi hivyo.
Kaimu Waziri wa Afya wa nchi hiyo James Hoth Mai, alisema siku ya Ijumaa kuwa, mtu huyo alikutwa na dalili za homa, vipele na mwili kuwashwa.
“Wizara ingependa kuutarifu umma juu ya mlipuko wa mpox,” alisema Waziri huyo wakati akizungumza na waandishi wa habari kutoka mji mkuu wa nchi hiyo, Juba.
Kulingana na Mai, maabara kuu ya nchi hiyo ilimfanyia vipimo raia mmoja wa Uganda ambaye pai ni mkazi wa eneo la kambi ya Kupuri, iliyoko Luri Payam, jijini Juba na kumkuta na dalili hizo.
Waziri huyo amesema kuwa, mgonjwa huyo alisafiri kwenda Uganda, hivi karibuni.
Aidha, ameongeza kwa kusema kuwa Wizara ya Afya ya nchi hiyo imejipanga kuratibu namna ya kukabiliana na ugonjwa huo.
“Mgonjwa huyo amewekwa sehemu maalumu katika hospitali ya Gudele. Timu ya wataalamu iko kazini kwa ajili ya uchunguzi na ufuatiliaji zaidi kuhusiana na mlipuko wa ugonjwa huo,” aliongeza.
Mai amewataka wahudumu wa afya kujipanga kukabiliana na maradhi hayo na pia kutoa taarifa mapema pindi watakapohisi uwepo wa maambukizi zaidi.