Halmashauri ya safari za anga ya Sudan imeongeza muda wa marufuku ya ndege kupaa anga zake hadi Juni 15 huku mapigano yakiendelea kati ya jeshi la taifa na kikosi cha dharura (RSF).
Katika taarifa Jumatano, hamlashauri hiyo ilisema kuwa ndege za kupitisha msaada na zile za shughuli za uokozi zitaruhusiwa kupaa.
“Ndege za kuokoa watu zitaruhusiwa ilimradi wapate ruhusa kutoka kwa ofisi husika,” taarifa hiyo ilisema.
Halmashauri hiyo ilidokeza kuwa huenda marufuku hiyo ikaongezewa muda tena.
Mapigano yalizuka katika mji mkuu Khartoum mwezi Aprili yaliyosababisha kuharibiwa kwa mfumo wa kuongoza safari za ndege katika uwanja wa ndege.
Zaidi ya watu 800 wameuawa katika ghasia hizo huku wengine milioni 1.4 wakiachwa bila makao. Watu 350,000 wamevuka mipaka kuingia nchi jirani.
Jumatano, jeshi la taifa lilijiondoa kutoka kwenye mazungumzo ya kusitisha mapigano huku likishutumu wapainzani wake kwa kukiuka masharti ya mkataba. Kujiondoa kwao kumezua wasiwasi wa kuzidi mapigano.