Baadhi  ya video zimekuwa zikiwaonesha wabunge kuzungumza na simu wakati mijadala muhimu ikiendelea Bungeni,/ Picha TRT Afrika

Baadhi ya wananchi Mkoani Dodoma nchini Tanzania wamesifu hatua ya spika wa bunge la nchi hiyo Dk. Tulia Ackson ya kutishia kuwatimua baadhi ya wabunge watakaobainika kuongea na simu ndani ya ukumbi wa bunge wakati wa vikao vikiendelea.

Wananchi hao wamekiri kwamba matumizi ya simu bungeni ni ukosefu wa nidhamu na umakini na kusema marufuku hii huenda ikabadilisha mambo.

Wakati huo huo, baadhi wameshauri kuwepo na sheria ya kutoingia kabisa na simu ndani ya ukumbi wa bunge kama ilivyo kwa maeneo mengine muhimu.

“Tunatamani kuwepo na sheria ya kutoingia na simu bungeni ama kama ni kuwa nayo basi waache getini wakati wa kuingia kama ilivyo Ikulu,’’amesema Mwaksege Barnaba, mkazi wa Dodoma.

Hatua hii sasa huenda ikaongeza umakini zaidi kwa wabunge kusikiliza na kutoa maoni kwa niaba ya wananchi wao.

Katika katazo lake Dk. Tulia ambaye alionesha kukerwa kwa kitendo hicho aliwataka wabunge kutotumia simu wakati wa vikao kwani wanasababisha wageni wanaofika hapo kuondoka na picha isiyopendeza.

‘’Waheshimiwa wabunge, leo ni siku yetu ya mwisho, niwakumbushe tena, msiongee na simu Bungeni, yani mnalifanya hili bunge hata hao watu wanaokuja sijui wanajifunza nini kutoka kwenu,’’ alisema na kuongeza, ‘’Milango ipo sita kama kuna ulazima wa kuzungumza na simu nenda nje, usizungumze na simu Bungeni usiseme Mwalimu ameanza nitakutaja ili utoke nje,” alisisitiza Dkt Tulia.

Joseph Waitara, ambaye ni mbunge wa Jimbo la Tarime vijijini ameonekana kukubaliana ha hatua hiyo ya Spika hivyo kuwataka wabunge wenzake kujizuia kupiga simu hadi kuwepo na jambo la dharura litakalowalazimu kufanya hivyo.

Mara kadhaa baadhi ya video zimekuwa zikiwaonesha wabunge kuzungumza na simu wakati mijadala muhimu ikiendelea Bungeni, hali ilioonesha kuwakwaza baadhi ya wananchi.

Bunge hilo la 12 lililokuwa likiendelea na vikao vyake jijini Dodoma limeahirishwa leo na waziri Mkuu wa nchi hiyo Kassim Majaaliwa. Vikao vyengine vinatarajiwa kuanza tena mwezi Oktoba mwaka huu.

TRT Afrika